Klabu ya Real Madrid imetangaza kikosi chao kamili kitakachosafiri kuelekea London, Uingereza, kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (UEFA) dhidi ya Arsenal. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa katika uwanja wa Emirates leo saa nne usiku (saa 11:00 kwa saa za Uingereza).
Real Madrid haikufanikiwa kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye hatua ya makundi ya UCL msimu huu, ambapo walishinda michezo mitano na kupoteza mitatu. Hii iliwalazimu kucheza hatua ya mtoano ya 16 bora, ambapo walikutana na Manchester City. Baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwa 3-2 na wa pili kwa 3-1, walifuzu kwa hatua ya 16 bora. Katika hatua hiyo, walifanikiwa kuiondoa Atletico Madrid kwa mikwaju ya penalti.
Kuelekea mchezo huu muhimu dhidi ya Arsenal, Real Madrid imewajumuisha wachezaji wao nyota wote kwenye kikosi. Wachezaji kama Kylian Mbappé, Vinícius Júnior, Jude Bellingham, Rodrygo, na Federico Valverde wote wamesafiri na timu kuelekea London.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amesema wanaamini wanaweza kushinda michuano hii. "Tunaamini tunaweza kushinda, la sivyo tusingekuwa hapa. Tuko hapa kupigania mataji yote hadi mwisho. Ili kushinda, tunahitaji kujituma," alisema Ancelotti kwa matumaini.
Aliongeza: "Ninachotaka ni kujiandaa vizuri kwa mchezo, na tumefanya hivyo. Tunakabiliana na timu kamili ambayo inajua jinsi ya kucheza vizuri katika eneo lao la ulinzi na kudhibiti mabadiliko ya haraka. Tunahitaji kuwa na mbinu iliyo wazi na kuitekeleza."
Ancelotti pia alisisitiza umuhimu wa uzoefu katika michuano hii: "Uzoefu ni muhimu sana katika mashindano haya. Uzoefu unamaanisha kutokuogopa michezo kama hii, kukabiliana na shinikizo moja kwa moja."
Kikosi cha Real Madrid kwa Mchezo wa Robo Fainali ya Kwanza ya UCL Dhidi ya Arsenal:
Makipa: Thibaut Courtois, Fran González, Sergio Mestre
Mabeki: David Alaba, Lucas Vázquez, Jesús Vallejo, Fran García, Antonio Rüdiger, Raúl Asencio, Jacobo Ramón, Lorenzo Aguado
Viungo: Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, Federico Valverde, Luka Modrić, Arda Güler, Chema Andrés
Washambuliaji: Vinícius Júnior, Kylian Mbappé, Rodrygo, Endrick, Brahim Díaz, Gonzalo García
Mashabiki wa Real Madrid nchini Tanzania na kote ulimwenguni wana matumaini makubwa kuwa timu yao inaweza kupata matokeo mazuri ugenini dhidi ya Arsenal na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.