Zoezi la usafishaji wa kikosi ndani ya Klabu ya Simba linaendelea kushika kasi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, huku taarifa za uhakika zikieleza kuwa beki wa kati raia wa Cameroon, Che Fondoh Malone, ndiye mchezaji anayefuata kuwekwa kwenye mlango wa kutokea.
Inaelezwa kuwa Malone, ambaye alijiunga na Wekundu wa Msimbazi msimu uliopita, ameshindwa kumshawishi kocha Fadlu, ambaye katika ripoti yake ya kiufundi amependekeza aachwe na badala yake asajiliwe beki mwingine wa kati atakayeendana na falsafa yake ya uchezaji.
Habari kutoka ndani ya klabu zinaarifu kuwa tayari mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, USM Alger ya nchini Algeria, wameonyesha nia ya dhati ya kuiwania saini ya beki huyo. "Kuna timu kutoka Morocco na Algeria zote zimeonyesha nia, lakini USM Alger wako 'serious' zaidi. Simba inataka kumuuza, na kama mambo yatakwenda sawa, anaweza akajiunga nao," kilisema chanzo chetu.
Wakati panga likimkumba Malone, kocha Fadlu ameagiza uongozi uhakikishe unamlinda winga Joshua Mutale, akisema mchezaji huyo ni sehemu muhimu ya mipango yake ya msimu ujao na hataki aondoke.
Hadi sasa, Simba imeshaagana rasmi na wachezaji wawili wa kigeni, Fabrice Ngoma na Valentine Nouma. Akizungumzia mchakato mzima wa usajili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema uongozi unafanya kazi kimya kimya lakini kwa umakini mkubwa.
"Wachezaji wote tunaowahitaji tunamalizana nao. Wapo ambao tayari tumewasajili na muda ukifika tutaweka kila kitu wazi. Hatufanyi usajili kwa mihemko, tunajenga timu imara kwa ajili ya Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa," alisema Ahmed.