Pantev Afungia Timu Chumba cha Video: Aandaa Mfumo Maalum wa 'Kipigo Kitakatifu' kwa Petro de Luanda

sports | Mon Nov 17 2025


Pantev Afungia Timu Chumba cha Video: Aandaa Mfumo Maalum wa 'Kipigo Kitakatifu' kwa Petro de Luanda

Kuelekea mtanange wa kwanza kabisa wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu ya Simba SC imegeuza uwanja wake wa mazoezi kuwa 'maabara' ya mbinu, huku Meneja Mkuu, Dimitar Pantev, akiwa amedhamiria kuanza kampeni hiyo kwa kishindo cha mabao mengi. Mchezo huo dhidi ya wababe wa Angola, Petro de Luanda, unatarajiwa kupigwa Novemba 23, 2025, saa kumi kamili jioni katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Habari za uhakika kutoka ndani ya kambi ya Wekundu wa Msimbazi zinaeleza kuwa Pantev hataki ushindi wa 'bahati nasibu' au bao moja la 'shida'. Mbulgaria huyo anataka 'mvua ya mabao'. Ili kufanikisha hili, amejifungia na wachezaji wake katika chumba cha video, akifanya uchambuzi wa kina wa 'fremu kwa fremu' jinsi Waangola hao wanavyocheza.


Taarifa zinaeleza kuwa Pantev amewasoma wapinzani wao na kugundua kuwa ngome yao kuu ipo katika safu ya kiungo na ulinzi. Hata hivyo, kama ilivyo kwa timu yoyote, amegundua pia 'nyufa' na udhaifu wao ambao anaamini ndio ufunguo wa kuwamaliza. Lengo lake ni kutumia udhaifu huo kuwapiga mabao mengi iwezekanavyo ili kujiweka pazuri mapema kwenye msimamo wa kundi.


Katika kuthibitisha hili, mfumo wa ushindi mnono wa mabao 6-0 alioutumia katika mchezo wa ligi juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, unaonekana kuwa ndio silaha anayoinolea kwa ajili ya Petro de Luanda. Mfumo huo ulioundwa kuleta 'kimbunga' cha mashambulizi, sasa unaboreshwa ili kuja 'kuwavuruga' kabisa viungo na mabeki wa Waangola hao, na kuwalazimisha kufanya makosa yatakayozaa mabao.


"Kocha amewaonyesha wachezaji video za jinsi Petro wanavyosambaza mipira na wachezaji wao muhimu wa kuchungwa," kilieleza chanzo chetu cha ndani. "Anachokifanya sasa ni kuwaandaa viungo wetu kucheza 'kamikaze', kuhakikisha viungo wa Petro hawafurukuti wala kupumua. Anataka kuua injini yao kwanza, kisha kuwashambulia."


Zaidi ya mbinu za kiufundi, Pantev ametoa maagizo makali kwa safu yake ya ushambuliaji. Amewataka wamalize 'utoto' wa kutumia vibaya nafasi. Amesisitiza kuwa katika mchezo huu wa kimataifa, kila nafasi inayopatikana karibu na lango la mpinzani lazima igeuzwe kuwa bao. Anataka 'clinical finishing' kwa asilimia mia moja, kwani anaamini ushindi wa mabao mengi utawapa heshima na kuanza kuongoza kundi, jambo litakalowapa mwelekeo mzuri kwa mechi zijazo.


Petro de Luanda si timu ya kubeza. Hivi sasa wanashika nafasi ya nne kwenye ligi yao ya Angola (Girabola) wakiwa na pointi 12 baada ya mechi sita. Wamefunga mabao 10 na kuruhusu matano. Hata hivyo, katika mchezo wao wa mwisho uliopigwa Novemba 9, walipokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa C.D. Primeiro de Agosto, timu ambayo Simba inaikumbuka vizuri kwani iliwahi kucheza nayo mwaka 2022.


Wakati Pantev akinoa makucha ya wachezaji, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally, amewasha 'moto' kwa mashabiki. Ahmed amesema maandalizi yanakwenda vizuri na sasa ni zamu ya 'Mnyama' (mashabiki) kujitokeza kwa wingi kuujaza Uwanja wa Mkapa na kuwatetemesha Waangola.


"Uwanja wa Benjamin Mkapa ulijengwa kwa ajili ya Simba. Tunaendelea kubaki peke yetu hapa na lazima tuwaonyeshe wageni wetu kuwa hapa si mahali salama kwao," alitamba Ahmed. "Wanaijua presha ya Mkapa; ile amsha amsha, zile kelele za kuwazomea wao na kuwashangilia sisi, zinawachanganya sana. Tunataka pande zote nne za uwanja ziwe za moto kwao."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.