Jioni ya Jumapili, tarehe 11 Mei 2025, ilishuhudia moja ya mechi za El Clásico zenye drama na mabao mengi zaidi katika miaka ya hivi karibuni, wakati FC Barcelona walipoibuka kidedea kwa kuichapa Real Madrid mabao 4-3 katika mchezo wa kusisimua wa La Liga. Mtanange huo, uliopigwa katika uwanja wao wa muda wa Estadi Olímpic Lluís Companys jijini Barcelona, ulikuwa ni wa mzunguko wa 35 wa ligi msimu wa 2024-2025, na ushindi huo umewasogeza Barcelona hatua moja tu karibu na kutwaa taji la La Liga baada ya miaka miwili.
Ushindi huu muhimu umewafanya Barcelona kufikisha alama 82 (mechi 26 za ushindi, sare 4, vipigo 5), wakiwaacha mahasimu wao Real Madrid na alama 75 (mechi 23 za ushindi, sare 6, vipigo 6), hivyo kuweka pengo la alama saba. Huku zikiwa zimesalia mechi tatu tu kumaliza msimu, Barcelona wanahitaji ushindi mmoja tu, au Real Madrid kupoteza mchezo mmoja, ili kujihakikishia ubingwa huo unaosubiriwa kwa hamu.
Msimu huu umekuwa wa kipekee kwa Barcelona dhidi ya Real Madrid, kwani wameshinda mechi zote nne za El Clásico walizokutana. Mbali na ushindi huu wa ligi, waliwanyuka Real Madrid mabao 4-0 katika mchezo wa La Liga mwezi Oktoba mwaka jana. Pia, waliwafunga tena mabao 5-2 kwenye fainali ya Supercopa de España mwezi Januari, na kuongeza kipigo cha mabao 3-2 katika fainali ya Copa del Rey mwezi Aprili, ambapo walitawazwa mabingwa.
Kiburi kikubwa kwa Barcelona ni idadi ya mabao waliyowafunga Real Madrid msimu huu – jumla ya mabao 16 katika mechi nne za El Clásico. Hii ni rekodi mpya kwa timu yoyote kuwahi kuifunga Real Madrid katika msimu mmoja, ikivunja rekodi ya awali ya mabao 13 iliyowekwa na Espanyol msimu wa 1929-1930 na Barcelona wenyewe msimu wa 2011-2012.
Mchezo wenyewe ulianza kwa kasi huku Real Madrid wakionekana kutawala dakika za mwanzo. Mshambuliaji wao mpya, Kylian Mbappé, aliwapatia wageni bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 5 tu ya mchezo. Mbappé aliendeleza maajabu yake kwa kufunga bao la pili dakika ya 14, akimalizia pasi safi kutoka kwa Vinícius Júnior, na kuiweka Real Madrid mbele kwa mabao 2-0.
Hata hivyo, Barcelona hawakukata tamaa. Walijibu mapigo vikali na kufanikiwa kubadili matokeo kabla ya mapumziko kwa kufunga mabao manne mfululizo. Eric García alianza kufungua ukurasa wa mabao kwa Barcelona dakika ya 19. Kinda wao mahiri, Lamine Yamal, alisawazisha dakika ya 32, na kuzidisha msisimko. Mshambuliaji Raphinha alikuwa moto wa kuotea mbali, akifunga mabao mawili ya haraka dakika ya 34 na dakika ya 45, na kuipeleka Barcelona mapumzikoni wakiwa mbele kwa mabao 4-2.
Raphinha amekuwa mwiba mchungu kwa Real Madrid msimu huu, akifunga jumla ya mabao matano na kutoa asisti mbili katika mechi nne alizocheza dhidi yao. Rekodi yake inafuatia ile ya Lionel Messi (sasa Inter Miami) ambaye alikuwa na jumla ya michango 8 ya mabao (goals + assists) katika El Clásico za msimu wa 2011-2012.
Kipindi cha pili, Kylian Mbappé alikamilisha ‘hat-trick’ yake dakika ya 70 na kufanya matokeo kuwa 4-3, lakini haikutosha kuiepusha Real Madrid na kipigo. Licha ya kufunga mabao matatu, Mbappé aliondoka uwanjani akiwa mnyonge. Hata hivyo, mabao hayo yalimfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji wa Real Madrid aliyefunga mabao mengi zaidi katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo, akiwa na jumla ya mabao 38 katika mechi 53 rasmi, akivunja rekodi ya Ivan Zamorano ya mabao 37 ya msimu wa 1992-1993.
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, alionyesha furaha yake baada ya mchezo: "Sijui nini kitatokea, lakini tuko katika nafasi nzuri ya kushinda ubingwa. Tunahitaji alama mbili zaidi. Tunataka kushinda haraka iwezekanavyo." Aliongeza kwa utani kuhusu timu yake kuruhusu mabao mawili ya mapema kabla ya kusawazisha: "Haikuwa burudani kwangu (kuruhusu mabao mawili ya mapema), wakati mwingine inaleta maumivu. Lakini nina furaha."
Ushindi huu wa El Clásico unamaanisha Barcelona sasa wako kileleni na wanahitaji tu matokeo mazuri katika mechi zao tatu zilizosalia ili kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa La Liga, na kurudisha heshima yao katika soka la Uhispania.