Aibu ya Taifa? Serikali Yaingilia Kati Skendo za Yamal, Adaiwa Kuwadhalilisha Walemavu Kwenye Sherehe

sports | Wed Jul 16 2025


Aibu ya Taifa? Serikali Yaingilia Kati Skendo za Yamal, Adaiwa Kuwadhalilisha Walemavu Kwenye Sherehe

Mambo yanazidi kuwa mabaya kwa nyota kinda wa soka, Lamine Yamal, kwani skendo zinazomwandama sasa zimefikia ngazi ya serikali. Wizara ya Haki za Kijamii ya Hispania imeamuru uchunguzi ufanyike kuhusu sherehe ya kutimiza miaka 18 ya mchezaji huyo wa Barcelona, kufuatia madai mazito kwamba aliwaajiri watu wenye ulemavu wa ufupi (udwarfism) kama sehemu ya burudani, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria nchini humo.


Utata huu mpya ulilipuka baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu wenye ufupi wakiwasili kwenye sherehe hiyo ya faragha iliyofanyika nje ya jiji la Barcelona. Nchini Hispania, ni marufuku kuwaajiri watu wenye ulemavu wa aina hiyo kwa ajili ya maonyesho yanayoweza kuwadhalilisha au kuwafanya kichekesho. Serikali sasa inataka ofisi ya mwendesha mashtaka na asasi za haki za binadamu zichunguze iwapo sheria za kulinda utu wa watu wenye ulemavu zilivunjwa.


Chama cha Watu Wenye Ufupi na Matatizo ya Mifupa (ADEE) kimetoa tamko kali, kikisema "Yamal amekiuka sheria zilizopo na maadili ya msingi," na kuahidi kuchukua hatua za kijamii kulinda heshima ya wanachama wao.


Skendo hii inakuja juu ya ile ya awali, ambapo mwanamitindo Claudia Calvo alidai kuwa aliombwa na upande wa Yamal alete wanawake 12 kwenye sherehe hiyo, huku akipewa vigezo maalum vya sura na maumbile yao, ikiwemo ukubwa wa kifua na rangi ya nywele. Calvo alidai kuwa wasichana hao pia wangepewa kadi zenye kiasi kikubwa cha pesa.


Kana kwamba hiyo haitoshi, maisha binafsi ya Yamal wakati wa likizo yamegubikwa na utata mwingine. Picha zilisambaa zikimwonyesha akifurahi na mwanamitindo mwenye umri wa miaka 29, Paty Basques, ambaye inasemekana ana mpenzi wake. Vilevile, mwanamitindo wa mtandao wa OnlyFans, Claudia Bavel, alidai kuwa Yamal alikuwa akimtumia ujumbe mara kwa mara licha ya yeye kumkatalia, madai ambayo Yamal ameyakanusha vikali akisema anasingiziwa.


Lamine Yamal anatajwa kama nyota ajaye atakayerithi mikoba ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Hata hivyo, mfululizo huu wa matukio ya ajabu nje ya uwanja umeanza kuwatia wasiwasi mkubwa mashabiki wake, wakihoji kama nidhamu yake binafsi itaweza kuendana na kipaji chake cha kipekee uwanjani.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.