Aibu! Kocha wa Nigeria Atupia Lawama Kwenye 'Juju', Adai DRC Waliwaroga Kwenye Penati

sports | Tue Nov 18 2025


Aibu! Kocha wa Nigeria Atupia Lawama Kwenye 'Juju', Adai DRC Waliwaroga Kwenye Penati

Uwanja wa soka barani Afrika umeshuhudia visa na mikasa mingi, lakini kile kilichotokea baada ya mchezo wa Nigeria dhidi ya DRC kimeacha ulimwengu wa soka vinywa wazi. Vigogo wa soka la Afrika, Nigeria 'Super Eagles', wamepata aibu ya pili mfululizo ya kukosa Fainali za Kombe la Dunia, lakini kocha wao mkuu, Eric Chelle, ametoa kisingizio ambacho hakikutarajiwa: "Tumerogwa".


Katika mchezo huo wa mtoano wa kuwania nafasi ya kwenda 'playoffs' za mabara, uliopigwa nchini Morocco, Nigeria (inayoshika nafasi ya 41 kwa ubora duniani) walikutana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC (nafasi ya 60). Licha ya Nigeria kujaa mastaa wao wote, walilazimishwa sare ya 1-1 hadi mwisho wa dakika 120 za mchezo. Mshindi alilazimika kupatikana kwa mikwaju ya penati, na hapo ndipo mambo yalipoharibika kwa Nigeria, wakifungwa 4-3.


Kipigo hiki kinamaanisha kuwa Nigeria, taifa lenye majigambo mengi kisoka, sasa limekosa Kombe la Dunia mara mbili mfululizo, baada ya kukosa pia lile la Qatar mwaka 2022. Kwa upande wa DRC, wanaendelea na safari ya kuelekea mtoano wa mwisho wa mabara.


Badala ya kukubali matokeo na kuwapongeza washindi, Kocha Mkuu wa Nigeria, Eric Chelle, aliamua kutoa lawama nzito mbele ya waandishi wa habari. Kwa mujibu wa kituo cha habari cha ESPN, Chelle alidai kuwa wachezaji wa DRC walikuwa wakitumia nguvu za giza, au 'Juju' (uchawi), ili kuwachanganya wachezaji wake wakati wa upigaji penati.


Chelle alitumia neno la Kiafrika Magharibi "Maraboutage", akimaanisha vitendo vya kishirikina vilivyokuwa vikifanywa na wapinzani wao.


"Kila penati ilipokuwa ikipigwa, watu wa DRC walikuwa wakifanya mambo yao ya Voodoo," alisema kocha huyo kwa hasira. "Nadhani hiyo ilitufanya tuwe na wasiwasi kidogo." Aliongeza kwa msisitizo: "(Ninyi waandishi wa habari) mmeona, siyo? Walikuwa wakinyunyiza maji au kitu gani sijui, na kufanya vitendo vya ajabu (huku akiigiza kwa mikono yake)."


Hata hivyo, waandishi wa ESPN waliripoti kuwa walipomuuliza aeleze kwa undani alichokiona hasa kilichokuwa ni uchawi, Kocha Chelle alishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha. Badala yake, aliishia kutikisa mkono wake wa kulia hewani, bila kueleweka wazi anamaanisha nini hasa.


Huu ni mchezo wa lawama ambao hauwezi kufuta ukweli kwamba DRC sasa wako hatua moja karibu na ndoto yao. Wakifanikiwa kushinda mtoano wa mabara (ambapo nchi 6 zitapigania nafasi 2 za mwisho), watakuwa wanarejea kwenye Kombe la Dunia kwa mara ya pili tu katika historia yao. Mara ya kwanza na ya mwisho ilikuwa mwaka 1974 nchini Ujerumani Magharibi, wakati huo wakishiriki kwa jina la Zaire.


Wakati Nigeria wakitafuta mchawi wa kuwalaumu, DRC wanaendelea na safari yao ya kupeperusha bendera ya Afrika.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.