Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka viongozi wa upinzani nchini Tanzania kuacha kulaumu serikali kuhusiana na kuzuiwa kwao kuingia nchini Angola. Kauli yake imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kuzuiwa na mamlaka za Angola kuingia nchini humo mnamo Machi 13.
Akizungumza na wanachama wa CCM katika mkutano uliofanyika Vwawa, wilayani Mbozi, mkoani Songwe, Wasira alisisitiza kuwa suala hilo halihusiani na serikali ya Tanzania, kwani hatua hiyo ilichukuliwa na mamlaka za Angola.
"Leo nimesoma kuwa baadhi ya viongozi walikuwa wanaelekea Angola, lakini wakanyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo. Hilo ni suala la Angola, si la Tanzania. Hapa hatujawapokonya pasipoti, na hata muda wake ukimalizika tunawapatia mpya waende wanakotaka na kurejea salama," alisema Wasira.
Aliongeza kuwa malalamiko yanayotolewa kuhusu ukimya wa serikali hayana msingi, kwani Tanzania haina mamlaka juu ya uwanja wa ndege wa Angola. "Angola ina taratibu zake. Inawezekana walikuwa na sababu zao za kuchukua hatua hiyo. Kama wangeuawa huko, si wangetulaumu kuwa kwanini hatukuingilia kati?" alihoji.
Mbali na Othman na Lissu, viongozi wengine waliokumbwa na hali hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro, jijini Luanda, ni marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho, pamoja na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Viongozi hao walikuwa wakielekea Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD), yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation, kwa lengo la kujadili demokrasia na kubadilishana uzoefu.
Wasira alisisitiza kuwa serikali ya Tanzania inaheshimu uhuru wa mataifa mengine na haingilii masuala ya ndani ya nchi nyingine. Aliongeza kuwa viongozi wa upinzani wanapaswa kuelewa kuwa kila nchi ina taratibu zake na kwamba ni muhimu kuzifuata.
Kauli ya Wasira imezua mjadala mkali katika medani za siasa nchini Tanzania, huku baadhi ya wachambuzi wakikubaliana naye na wengine wakipinga. Hata hivyo, Wasira amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania haina hatia katika suala hilo na kwamba viongozi wa upinzani wanapaswa kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa mamlaka za Angola.