Makalla: Tanzania Haina Shinikizo la Kuruhusu Wageni, Karua Azuiwa kwa Sheria

politics | Tue May 20 2025


Makalla: Tanzania Haina Shinikizo la Kuruhusu Wageni, Karua Azuiwa kwa Sheria

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amejibu kelele zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuzuiwa kuingia nchini kwa mwanaharakati Martha Karua wa Kenya na wenzake. Makalla amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi huru, yenye mamlaka kamili, na haiwezi kulazimishwa kuruhusu mtu yeyote kuingia kwa shinikizo kutoka nje.


Akizungumza na wananchi wa Mji wa Katoro, mkoani Geita, katika mkutano wa hadhara wakati akiendelea na ziara yake ya siku saba, Makalla alisema kuwa watu wote wenye hila na mipango ya uchochezi ya kuwagawa Watanzania hawana nafasi katika taifa hilo. “Hata hili nafikiri nilisemee hapa, kwenye mitandao ya kijamii tunaona heeh sijui mwanaharakati Martha Karua wamezuiwa uwanja wa ndege walikuwa wanakuja kwenye kesi ya Tundu Lissu. Nataka niseme, Tanzania hii ni nchi huru, ni dola iliyokamilika, yenye mamlaka kamili, inayouwezo wa kuruhusu au kutoruhusu mgeni yeyote kuingia Tanzania,” alisema Makalla.


Alisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kulazimishwa kuruhusu mtu yeyote kuingia kwa shinikizo, akiongeza kuwa hakuna sheria yoyote duniani inayoweza kulishinikiza taifa huru, likiwamo Tanzania, kwamba washinikize mtu fulani apokewe. “Hawawezi kulazimishwa kwa kuwa Tanzania ni nchi huru, yenye dola kamili na yenye mamlaka kamili, haiwezi kuruhusu hilo kwa shinikizo kwamba, ‘tunaomba huyu aruhusiwe kuingia Tanzania’,” alisisitiza Makalla.


Makalla alieleza kuwa Idara ya Uhamiaji ina mamlaka ya kuruhusu au kutoruhusu mtu wa kigeni kuingia nchini kwa sababu wanazingatia sheria na kanuni. Alifafanua kuwa mwanaharakati huyo ana rekodi nchini Kenya ambazo hazijafutwa, na Tanzania kama nchi salama na ya mfano, haiwezi kuruhusu mtu mwenye rekodi kama hizo kuingia. “Tumemshtukia, tumeshtuka yeye ni mwanaharaki wana rekodi Kenya hazijafutwa, Tanzania ni nchi salama na ya mfano, uhusiano wetu na Kenya ni wa kihistoria tutaendelea kushirikiana na Wakenya na si kwa sababu ya Martha Karua, mahusiano ni mazuri kuliko wakati wowote na sisi ni ndugu,” alisema.


Kauli hii inakuja wakati ambapo kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa nchi katika kusimamia sheria zake, hasa katika suala la kuingia kwa wageni. Serikali imesisitiza kuwa sheria za nchi lazima zifuatwe na kila mtu, bila kujali asili yake au madhumuni ya ziara yake.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.