Serikali ya Kenya imesema kuwa Tanzania ilikuwa na haki ya kufanya uamuzi wa kuwazuia watu kadhaa wa kisiasa na wanaharakati wa Kenya, wakiongozwa na Martha Karua, kuingia nchini. Msemaji wa serikali ya Kenya, Isaac Mwaura, amesema kuwa Kenya haikuhusika wala haina jukumu lolote katika uamuzi huo wa Tanzania.
Mwaura aliyasema haya leo alipokuwa akijibu kuhusu hatua ya kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu, Martha Karua, Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga, na wanaharakati wengine wanne kuzuiwa kuingia Tanzania siku chache zilizopita. Inaripotiwa kuwa Karua na wenzake walikuwa na lengo la kuingia nchini Tanzania kwa ajili ya kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambayo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Ikiwa serikali ya moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaamua kumkataa mtu binafsi kuingia nchini mwao, ina mamlaka ya kufanya hivyo,” alisema Mwaura. Alisisitiza kuwa serikali ya Kenya inaheshimu uhuru wa nchi wanachama wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na haiingilii maamuzi yao ya ndani.
“Ikiwa wameamua hivyo, huo ni uamuzi wao. Hatujui kwa nini watamzuia mtu, na serikali ya Kenya haihusiki,” aliongeza Mwaura.
Siku ya Jumapili iliyopita, Martha Karua na wengine wawili walirudishwa nchini Kenya mara baada ya kuwasili Tanzania, wakati Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga, pamoja na wanaharakati wa haki Hussein Khalid na Hanifa Adan, walizuiliwa walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Tukio hili limezua mjadala miongoni mwa wananchi na wadau wa siasa katika nchi zote mbili.