Vijana Songwe Wafunguka kwa Waziri Nanauka, Wasomi wa UDOM Waomba Mitaji

politics | Wed Nov 26 2025


Vijana Songwe Wafunguka kwa Waziri Nanauka, Wasomi wa UDOM Waomba Mitaji

Mkoani Songwe, hali ya hewa ya kisiasa na kiuchumi imeanza kubadilika, huku vijana wakionyesha matumaini mapya kufuatia uamuzi wa kimkakati wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuunda Wizara maalum itakayosimamia Maendeleo ya Vijana. Hatua hii imepokelewa kwa vifijo na nderemo katika wilaya ya Songwe, ikitajwa kama "mwarobaini" wa changamoto sugu za ukosefu wa ajira na mitaji.


Hayo yamebainika leo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Mhe. Joel Nanauka, alipotembelea maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwemo soko la Mkwajuni na migodi ya Saza ili kusikiliza kero za vijana ana kwa ana.


Kilio cha Bodaboda na Bima za Afya Katika mkutano uliowakutanisha makundi mbalimbali, vijana wanaoendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda katika eneo la Mkwajuni, walipaza sauti zao wakitaka serikali isiishie kwenye ofisi za kifahari bali ishuke chini kuwatatulia kero za msingi.


Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Mkwajuni, Hamisi Jairi, alimueleza Waziri kuwa vijana wengi wanafanya kazi hiyo kwa "kubangaiza" kutokana na kukosa mafunzo rasmi. "Mheshimiwa Waziri, tunapenda kuwa madereva bora, lakini vyuo vya udereva huku kwetu ni adimu. Tunaiomba wizara yako mpya ituletee vyuo vya ufundi ili tupate leseni halali na kuepuka kukimbizana na trafiki kila siku," alisema Jairi.


Aliongeza kuwa, mbali na leseni, vijana hao wanatamani kuunganishwa katika mfumo rasmi wa Bima ya Afya (NHIF) ili wawe na uhakika wa matibabu pindi wanapougua au kupata ajali, jambo ambalo kwa sasa ni mtihani mgumu kwao.


Wasomi wa Vyuo Vikuu 'Wakiwasha' Sokoni Uhalisia wa maisha ya mtaani umedhihirika baada ya Zacharia Matogoro, kijana msomi na mhitimu wa Shahada ya Lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2022, kujitokeza na kueleza namna anavyopambana sokoni badala ya kukaa ofisini kusubiri ajira. Matogoro, ambaye sasa ni mjasiriamali katika soko la Mkwajuni, amemwomba Waziri kumtazama kwa jicho la huruma yeye na wenzake wenye uthubutu.


"Mheshimiwa, elimu ninayo lakini mtaji ni changamoto. Nimejiajiri hapa sokoni lakini miundombinu si rafiki na mtaji ni mdogo. Nikiwezeshwa mkopo wa kati ya Shilingi Milioni 3 hadi 4, nina uhakika wa kukuza biashara hii, kuajiri wengine na kurejesha mkopo huo bila shida," alieleza msomi huyo kwa kujiamini.


Wachimbaji Wadogo Saza Wataka Viwanda Kule katika kijiji cha Saza, maarufu kwa shughuli za madini, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Shadrack Mwakyalyabwe, amesema vijana wamechoka kuwa vibarua wa kuchimba na kuuza mali ghafi. Ametoa wito kwa serikali kuwapa mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo vya kuchenjulia na kuongeza thamani madini ili fedha ibaki mikononi mwa wazawa.


Ahadi ya Siku 100 na Maagizo kwa Halmashauri Akijibu hoja hizo nzito, Waziri Nanauka amewatoa hofu vijana hao na kutangaza neema inayokuja. Ametoa agizo kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, ikiwemo ya Songwe, kuanza mara moja kuandaa mazingira wezeshi ya kupokea fedha za uwezeshaji.


"Rais Samia hataki maneno mengi, anataka matokeo. Ndani ya siku 100 za uongozi huu mpya, kuna fedha maalum zimetengwa kwa ajili ya kuwakwamua vijana. Nataka Halmashauri zijiandae ili fedha hizi zikiingia, ziwafikie walengwa bila urasimu wala mizengwe," alisisitiza Waziri Nanauka.


Alihitimisha kwa kuwataka vijana kuendelea kuwa wabunifu na wazalendo, akisema kuwa maono ya Rais ni kuona nguvukazi ya taifa inashiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na siyo kuwa watazamaji wa uchumi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.