Mji wa kibiashara na mpakani wa Tunduma mkoani Songwe, jana ulisimama kwa muda kupisha ziara ya kishindo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Mhe. Joel Nanauka. Ziara hiyo iliyolenga kuwasha mwenge wa matumaini kwa vijana, iligeuka kuwa jukwaa la "kufunguka" huku serikali ikitangaza mapinduzi ya kidijitali katika kutatua kero za kundi hilo kubwa nchini.
Akiwa ameambatana na wenyeji wake, Waziri Nanauka alitangaza habari njema ambayo imepokelewa kwa shangwe; mpango wa serikali wa kuanzisha mfumo maalum wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Mfumo huo unatajwa kuwa utakuwa kiunganishi cha moja kwa moja kati ya "kijana wa mtaani" na serikali yake, ukiondoa urasimu wa kizamani wa kusubiri barua au miadi ya kuonana na vigogo.
Simu Yako, Ofisi Yako "Dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuona kijana hasote kufikisha wazo au kilio chake. Kupitia mfumo huu wa kidijitali, kijana akiwa kijiweni kwake au shambani, atatuma wazo lake, ushauri au changamoto na serikali itazipokea na kuzifanyia kazi kwa kasi ya '5G'. Hii ndiyo maana halisi ya kuwa na Wizara maalum kwa ajili yenu," alisisitiza Nanauka huku akishangiliwa.
Alibainisha kuwa mfumo huo utakuwa suluhisho la kudumu la 'ukimya' wa vijana wengi ambao wamekuwa wakikosa pa kusemea, na hivyo kuwafanya wajihisi wametengwa katika mnyororo wa maendeleo ya taifa.
Tunduma 'Yafunguka' kwa Uchungu Hata hivyo, mkutano huo haukuisha kwa hotuba laini pekee. Hali ya hewa ilibadilika pale vijana wa mji wa Tunduma, maarufu kwa harakati za biashara, walipopewa nafasi ya kutema nyongo. Kilio kikubwa kilichotawala ni "mkono mzito" wa Jeshi la Polisi dhidi yao, hususan madereva wa bajaji na bodaboda.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Bajaji, Hamisi Mwinyi, alisimama kidete na kumueleza Waziri kuwa vijana wamegeuzwa "mtaji" na baadhi ya askari wasio waaminifu. "Mheshimiwa Waziri, hapa Tunduma tunaishi kwa mashaka. Ukijaribu kutoa hoja au kudai haki yako, unakamatwa na kuwekwa ndani bila sababu za msingi. Tunanyanyaswa tunapoutafuta mkate wetu wa kila siku," alilalamika Mwinyi kwa hisia kali.
RC Makame Atibua 'Dili' za Checkpoint Akijibu mapigo hayo papo hapo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Jabir Makame, alionyesha ukomavu wa uongozi kwa kukiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuchukua hatua za papo kwa hapo. RC Makame alikiri kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakikamatwa, lakini akafafanua kuwa mara nyingi ni kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani, kama vile kuweka taa zenye mwanga mkali (spotlights) na mapambo yanayokwaza watumiaji wengine wa barabara.
Hata hivyo, katika kutenda haki, RC Makame alipiga marufuku mara moja tabia ya askari kutoza fedha kiholela kwenye vituo vya ukaguzi (checkpoints). "Kuanzia sasa, sitaki kusikia askari anageuza kituo cha ukaguzi kuwa sehemu ya kudai rushwa au tozo zisizo rasmi. Hilo ni kosa na halivumiliki. Tunataka vijana wafanye kazi, lakini wafuate sheria," aliamuru Mkuu huyo wa Mkoa.
Akihitimisha mjadala huo, Waziri Nanauka aliagiza uongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma kumaliza kero hizo mezani haraka iwezekanavyo. Alisisitiza kuwa lengo la serikali ni kutengeneza mazingira rafiki ili vijana waweze kuchangia pato la taifa badala ya kushinda vituo vya polisi.