Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imemaliza rasmi ziara yao iliyojulikana kama ‘Mama Full Box Oparesheni’ kwa kufanya mikutano mikubwa ya hadhara katika kata za Ibinzamata na Kitangili. Ziara hii ilikuwa na lengo kuu la kuwahamasisha wananchi kujiandaa kikamilifu kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Katika hotuba yake wakati wa hitimisho la ziara hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Sakala, alieleza jinsi vijana walivyoguswa na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake. Alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na maendeleo kwa wananchi umeonekana wazi.
"Ndugu zangu, Rais Samia ndani ya miaka minne ya dhahabu amefanikisha miradi mikubwa kama Daraja la Busisi, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya SGR, na hapa Shinyanga tumeona ujenzi wa Uwanja wa Ndege. Tunataka aendelee kuongoza – Mitano Tena," alisema Sakala, akionyesha imani yao kwa Rais na chama chao.
Katibu wa UVCCM Wilaya hiyo, Naibu Katalambula, aliwataka wananchi kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kufuata katiba ya nchi. Aliwahimiza wapigakura kuwachagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge, hadi urais.
"Tutaendesha kampeni zetu kwa amani. Vijana na wananchi wote tunapaswa kupuuza propaganda za baadhi ya vyama vya upinzani vinavyolenga kuvuruga amani. Tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu," aliongeza Katalambula, akisisitiza umuhimu wa amani na utulivu wakati wa uchaguzi.
Diwani wa Ibinzamata, Ezekiel Sabo, alipongeza juhudi za UVCCM katika kueneza ujumbe wa maendeleo. Alisema kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM umefikia asilimia 85 katika kata yake, na miradi mingi imejikita katika ujenzi wa masoko na stendi ya kisasa ya mabasi.
Naye Diwani wa Kitangili, Mariamu Nyangaka, alieleza kuwa kata yake imepiga hatua kubwa katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, madaraja, na zahanati mpya. Alisisitiza kuwa maendeleo haya yameleta mabadiliko chanya kwa wananchi.
Ziara ya ‘Mama Full Box Oparesheni’ ilianza Aprili 5, 2025, na kuhitimishwa Aprili 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.