Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini umezindua rasmi kampeni ya kata kwa kata kwa lengo la kuhamasisha vijana, wanachama wa chama hicho, na wananchi kwa ujumla kujiandaa kikamilifu kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kampeni hii ina lengo la kuwashawishi wapiga kura wampigie kura nyingi Rais Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa CCM.
Ziara hiyo, iliyoanza hivi karibuni, inaendeshwa chini ya kauli mbiu ya "Mama Full Box Oparesheni," ambayo ina maana ya kuhakikisha kuwa kura za Rais Samia zinajaza kila sanduku la kura siku ya uchaguzi, ili aweze kupata ushindi wa kishindo na kuendelea kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo endelevu.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bw. Abdulazizi Sakala, akizungumza wakati wa ziara hiyo katika Kata ya Mwawaza, alieleza kuwa vijana wa CCM katika wilaya hiyo wanaunga mkono kwa dhati Azimio la Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, ambalo lilimpitisha Rais Samia kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, pamoja na Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
"Kutokana na kuunga mkono azimio hilo, tumeamua kuzindua kampeni hii ya kuhamasisha vijana, wanachama wa CCM, na wananchi kwa ujumla kujiandaa kikamilifu kwa uchaguzi mkuu," alisema Bw. Sakala. Aliongeza kuwa katika Kata ya Mwawaza, kuna maendeleo makubwa yanafanyika, ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambayo sasa inajengwa kwa kiwango cha lami.
Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bw. Naibu Katalambula, alitoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa zinazozagaa kuwa uchaguzi hautakuwepo, akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa. Aliwahimiza wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi za udiwani na ubunge mara tu kipenga cha uchaguzi kitakapolia, lakini akawaonya wajipime kwanza kama wana uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Ziara hiyo ya "Mama Full Box Oparesheni" pia inahusisha uzinduzi wa mashina ya mama katika kata mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha chama na kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.