Wakati Fumba, wilayani Magharibi B, Unguja, ikitajwa kama kitovu kipya cha uwekezaji wa utalii, kwa wakazi wake wa asili, maendeleo hayo yamegeuka kuwa janga linalozaa machozi na simanzi. Wananchi wameelezea masikitiko yao makubwa wakidai kuwa miradi ya utalii inawanyang'anya ardhi yao ya urithi na kuwaacha bila ajira wala matumaini.
Kilio hiki kiliibuka kwa nguvu katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambapo wananchi walifunguka kuhusu jinsi mashamba yao ya kilimo yanavyogeuzwa kuwa hoteli na makazi ya kifahari kwa wawekezaji. Hali hii imewapokonya si tu eneo la kulima, bali pia njia yao kuu ya kujipatia kipato na chakula.
"Ardhi niliyoachiwa na bibi zangu imechukuliwa na nimeachwa mikono mitupu," alisema Mama Halima Mzee, akielezea kwa uchungu jinsi urithi wa familia yake ulivyopotea. Simulizi yake inaakisi maumivu ya wengi wanaoshuhudia ardhi yao ikihodhiwa na wageni.
Kinachowaumiza zaidi, ni kwamba hata fursa za ajira zinazotokana na miradi hiyo haziwanufaishi. Vijana wa Fumba na Bweleo wanasema kazi nyingi zinapewa watu kutoka nje ya maeneo yao, na kuwaacha wao wakitanga-tanga bila ajira na kuwa mzigo kwa familia zao. Vilevile, wameeleza jinsi ukanda wa fukwe, ambao ni sehemu muhimu ya urithi na maisha yao ya kijamii, unavyoporwa na kuwekewa uzio na wawekezaji.
Akijibu kero hizo, Othman Masoud Othman alisema hali hiyo haikubaliki na ni lazima ifike mwisho. Alisisitiza kuwa rasilimali ya ardhi ya Zanzibar ni kwa ajili ya Wazanzibari kwanza, kabla ya mwekezaji mwingine yeyote. "Serikali ya ACT Wazalendo haitakubali kuona wananchi wake wakinyanyasika kwenye nchi yao wenyewe. Sera yetu ni kumlinda mwananchi kwanza. Si kila kipande cha ardhi ni cha kupewa mwekezaji, thamani ya mwananchi lazima iheshimiwe," aliahidi Othman.
Ahadi hiyo imeibua matumaini mapya kwa wakazi wa Fumba, ambao sasa wanaona suala la ardhi kuwa ajenda kuu itakayoamua mustakabali wao katika uchaguzi ujao.