Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameibua upya na kuahidi kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala la fidia kwa wananchi walioathirika na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba. Akizungumza kwa hisia kali mbele ya wakazi wa Shehia ya Furaha, Wilaya ya Chake Chake, Othman alieleza kusikitishwa kwake na kile alichokiita "uonevu na unyanyasaji" ambapo wananchi wanapokonywa haki zao za msingi za umiliki wa ardhi.
Alisema ni jambo lisilokubalika kwa serikali kuchukua mashamba ambayo yalikuwa tegemeo la maisha kwa familia nyingi na kisha kutoa malipo duni yasiyoendana na thamani halisi ya mali zao. "Huwezi kumchukulia mtu shamba lake alilokuwa analima na kupata riziki, kisha umpe kiasi kidogo cha fedha ambacho hakiwezi hata kuanzisha maisha mapya. Huu ni unyanyasaji unaoongeza umaskini kwa watu wetu na serikali yangu haitavumilia hili," alisisitiza Othman.
Alieleza kuwa amepokea malalamiko mengi, baadhi yakihusu wananchi ambao hawajalipwa kabisa, na wengine wakilalamikia kupewa fidia isiyoridhisha. Aliweka ahadi thabiti kwamba endapo atachaguliwa, atasimamia binafsi kuhakikisha kila mwananchi anayepisha mradi huo anapata fidia stahiki kulingana na tathmini halisi ya soko la ardhi wakati huo.
Kauli ya Othman ilifungua milango kwa wananchi kuelezea machungu yao. Abdalla Seif, mmoja wa waathirika, alisema fidia aliyopokea haikulingana hata kidogo na hasara aliyoipata baada ya shamba lake kuchukuliwa. Naye Ali Abdalla Juma alieleza kwa uchungu jinsi eneo lake lenye thamani inayoweza kufika Shilingi milioni 100 za Kitanzania lilivyolipwa fidia isiyozidi hata Shilingi milioni 50. "Hii ni dhuluma ya wazi. Tumeshalalamika sana lakini sauti zetu hazisikilizwi," alisema Juma.
Wananchi walimkabidhi Othman Masoud jukumu la kurejesha imani yao kwa serikali, wakimtaka ahakikishe uongozi wake unajikita katika msingi wa haki, usawa na uwajibikaji, hasa katika masuala yanayohusu ardhi na maisha ya watu.