Jukwaa la kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Lindi limegeuka kuwa uwanja wa mavuno ya kisiasa, baada ya wimbi la wanachama na viongozi waandamizi kutoka vyama vya upinzani kutangaza rasmi kurejea "nyumbani". Tukio hilo la aina yake lilitokea mbele ya mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, ambaye aliwapokea kwa mikono miwili huku akisisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa.
Miongoni mwa vigogo waliovua magwanda ya upinzani na kuvaa yale ya kijani ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Lindi Mjini, Salum Bar’wani, aliyekuwa mgombea ubunge wa CHAUMMA jimbo la Mchinga, Yusuph Tamba, na mtia nia wa ubunge jimbo hilo kupitia CUF, Rehema Muhema, ambaye aliamua kurejea CCM pamoja na mumewe.
Akielezea sababu za uamuzi wake, Bw. Bar’wani alisema amevutiwa na mwelekeo wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka huu, hasa katika dhamira yake ya kuufungua kiuchumi Mkoa wa Lindi. Alitaja mradi mkubwa wa gesi ambao umesubiriwa kwa takriban miaka 12, akionesha imani kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, mradi huo utakamilika. Cha kushangaza zaidi, alisema ahadi ya CCM ya kuleta Katiba Mpya, ambayo imekuwa ajenda kuu na kilio cha muda mrefu cha upinzani, imempa sababu tosha ya kuamini kuwa mapambano sasa yanapaswa kuendelezwa ndani ya CCM.
Kwa upande wake, Yusuph Tamba alisema ameamua kwa ridhaa yake mwenyewe kuunga mkono CCM na kwamba hatishwi na vitisho anavyodai amekuwa akipokea tangu aoneshe dalili za kuhama chama. "Mimi si mtoto mdogo, sitishiki tena. Nimeamua kurudi nyumbani," alisema kwa kujiamini.
Akitoa hotuba yake, Rais Samia alionyesha kufurahishwa na hatua hiyo, akisema maneno yaliyotolewa na wanachama hao wapya yana uzito mkubwa na yanaonesha ukomavu. Aliwakaribisha na kutoa wito kwa wengine ambao bado wana mashaka kuungana na CCM katika safari ya kujenga Tanzania yenja amani na mshikamano.
Tukio hili linatafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama pigo kwa vyama vya upinzani mkoani Lindi na ushindi mkubwa wa kimkakati kwa kampeni za CCM.