Utekelezaji wa mradi muhimu wa ujenzi wa barabara ya juu (flyover) katika maeneo ya Amani na Mwanakwerekwe, Zanzibar, umekumbwa na kashfa nzito, baada ya serikali kubaini kuwepo kwa 'watu hewa' kwenye orodha ya malipo na gharama za fidia kupaa na kuwa kubwa kuliko gharama ya ujenzi wa mradi wenyewe.
Hali hiyo imeilazimu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusitisha mchakato wa malipo na kuamuru kufanyika kwa tathmini ya pili na ya kina, ili kuwabaini wote waliojihusisha na njama hiyo ya kuiibia serikali.
Akizungumza na wanahabari jana, Julai 28, 2025, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhamed, alithibitisha kuwepo kwa dosari hizo, akisema hali ya gharama za fidia kuwa kubwa kuliko za mradi ni jambo linalotia shaka na lisilokubalika.
"Tumebaini kuna dosari kwenye tathmini ya awali. Ndiyo maana tumeamua kufanya tathmini ya pili ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wanaostahili na fedha za umma zinalindwa," alisema Dk. Khalid.
Akifafanua zaidi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema kuna dalili za kuwepo kwa mchezo mchafu unaohusisha baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu wanaoshirikiana na wananchi wachache. "Wamekuwa wakipandisha viwango vya fidia visivyo halali kwa lengo la kujipatia fedha za ziada na kugawana. Serikali haitavumilia hujuma hii," alisisitiza Dk. Mkuya.
Wakati serikali ikipambana na watu hewa, baadhi ya wananchi wanaostahili fidia wamelalamikia tathmini ya awali, wakidai viwango walivyopangiwa ni vidogo na haviendani na thamani halisi ya mali zao. Wamesema hawako tayari kuhama hadi watakapolipwa fidia stahiki.
Waziri Khalid amewataka wananchi wote wenye malalamiko halali kuwasilisha madai yao rasmi serikalini ili yashughulikiwe, badala ya kutoa kauli zinazoweza kuchelewesha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.