Dodoma: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amemuelekeza Katibu Mkuu, Utumishi, Juma Mkomi, kuhakikisha kuwa barua za ajira kwa watu waliofaulu usaili zinatolewa katika mikoa husika walikofanyia usaili. Agizo hili linabadilisha utaratibu wa awali ambao uliwalazimu waajiriwa hao kusafiri hadi Dodoma kwenda kuzichukua barua hizo kwenye Sekretarieti ya Ajira.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Waziri Simbachawene alisema kuwa utaratibu wa sasa unawagharimu waajiriwa, unawasumbua, na unapoteza muda wao.
Alitoa mfano wa mtu aliyefanya usaili katika Mkoa wa Kigoma ambaye anapaswa kusafiri hadi Dodoma kuchukua barua yake, kisha kurudi Kigoma au kwenda mkoa mwingine alikopangiwa kazi. Alisema kuwa hali hii si haki kwa waajiriwa hao wapya.
“Hii si sawa, kwani tunawasumbua na wanachoka hata kabla ya kuanza kazi. Tuwaonee huruma. Barua hizo wazichukulie kwenye mikoa walikofanyia usaili. Tuwape dhamana makatibu tawala wetu, ambao tunaamini wana uwezo na maadili ya kutekeleza jukumu hilo,” alisisitiza Waziri Simbachawene.
Alieleza kuwa angependa kuona waajiriwa wapya wakichukua barua zao katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa husika, badala ya kufanya safari zisizo za lazima kwenda Dodoma kabla ya kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi.