Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema mmoja wa watumishi wa umma aliyejihamisha kutoka Jeshi la Zimamoto na kujipeleka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) amefukuzwa kazi.
Akizungumza jijini Dodoma katika kikao kazi na Wakuu wa Taasisi za Umma, Simbachawene alieleza kuwa ofisi yake inaendelea kushughulikia mtandao wa kughushi barua za uhamisho serikalini. Alifafanua kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa kwa watumishi waliojipangia uhamisho kinyume cha utaratibu, ambapo mmoja wao tayari amepoteza ajira yake.
“Mmoja kati ya wale aliyejihamisha kutoka Zimamoto kwenda TPDC ni kijana ninayemfahamu, lakini kazi nzuri mmemfukuza. Nilipigiwa simu na huyo kijana akisema ‘Baba nimefukuzwa kazi, sitarudi tena kazini,’ nikamjibu, ‘Muombe Mungu, endelea huko huko,’” alisema Waziri Simbachawene.
Ameeleza kuwa hatua kama hizo ni muhimu katika kujenga misingi ya uadilifu serikalini na kuhakikisha kila mtumishi anafuata taratibu za ajira bila kulindana. Aidha, alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka ili kujinufaisha binafsi.
Serikali imekuwa ikidhibiti mianya ya ubadhirifu na utovu wa nidhamu miongoni mwa watumishi wa umma, huku ikihimiza uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma kwa ajili ya maslahi ya taifa.