Rais Samia Suluhu Hassan ametoa idhini ya kuongezwa kwa ajira mpya 300 katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na hivyo kufanya jumla ya ajira zote kuwa 1,896 kutoka 1,596 zilizotangazwa awali. Ongezeko hili linatokana na ombi la TRA la kuongeza nafasi za ajira 300, ambazo zilikuwa zimetengwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha ujao wa 2025/2026, ili zijazwe katika mchakato wa ajira uliohitimishwa hivi karibuni. Ombi hili limekubaliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Moshi Jonathan Kabengwe, kwa niaba ya Kamishna Mkuu, waajiriwa wapya 1,896 wa TRA watapokea barua zao za ajira leo, tarehe 28 Mei 2025, kupitia barua pepe zao.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa wasailiwa 1,896 waliofaulu na kuitwa kazini wanatakiwa kufika katika kumbi walizopangiwa tarehe 2 Juni 2025 saa 1:00 asubuhi bila kukosa, wakiwa na nyaraka muhimu kama zilivyoainishwa katika barua pepe zao.
Mamlaka inawashukuru waombaji wote walioonyesha nia ya kufanya kazi na Mamlaka ya Mapato Tanzania, na inawatakia kila la kheri katika ujenzi wa taifa. Aidha, taarifa za waombaji 4,429 walioshiriki usaili wa mahojiano na hawakufanikiwa kuitwa kazini zitahifadhiwa katika kanzidata ya Mamlaka kwa matumizi ya baadaye.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza nafasi za kazi zipatazo 1,596 mwanzoni mwa Februari 2025, na kupokea jumla ya maombi 135,027. Kati yao, 113,023 waliitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika baada ya kukidhi vigezo, na usaili huo ulifanyika tarehe 29 na 30 Machi 2025. Wasailiwa waliofaulu usaili wa kuandika waliitwa kwenye usaili wa mahojiano uliofanyika tarehe 12 hadi 14 Mei 2025, ambapo wasailiwa 6,325 walishiriki.
Hatua hii ya kuongeza ajira inaonyesha juhudi za serikali katika kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali. Pia, inaonyesha dhamira ya serikali katika kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.