Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito mzito kwa vyombo vya habari barani Afrika, akiviagiza kuwa mstari wa mbele katika kusimulia hadithi halisi ya Afrika kwa "sauti ya Kiafrika," ili kubadili masimulizi potofu na badala yake kuonyesha mafanikio, ubunifu, na mchango wa bara hili duniani.
Maagizo hayo ya Rais yametolewa jana jijini Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa kihistoria wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), ulioenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Katika hotuba yake, Rais Samia alielekeza maono yake katika nguzo tatu kuu kwa mustakabali wa habari barani. Kwanza, alitaka vyombo vya habari vijenge simulizi chanya linaloakisi uhalisia wa Afrika. "Hadithini kuhusu ubunifu wa vijana wetu, ujasiri wa wanawake wetu katika sayansi na teknolojia, na mchango wetu katika uchumi wa dunia," ilisema sehemu ya hotuba yake.
Pili, Rais alisisitiza umuhimu wa ujumuishi, akiviagiza vyombo vya habari kuhakikisha vinatenga muda na kuandaa programu maalum zinazozingatia makundi yote, hasa watu wenye ulemavu, wanawake, na watoto, ili sauti zao zisikike na hakuna anayebaki nyuma.
Tatu, alizungumzia changamoto ya zama za kidijitali, hasa matumizi ya Akili Mnemba (AI). Huku akitambua kuwa AI inaweza kurahisisha ukusanyaji na usambazaji wa habari, alionya kuhusu hatari yake katika kuzalisha taarifa za uongo. Alilitaka kongamano hilo kutoa mapendekezo ya kisera yatakayoliwezesha bara la Afrika kunufaika na AI bila kuathiri maadili ya uandishi na haki ya umma kupata taarifa sahihi.
Akizungumzia muktadha wa Tanzania, Waziri wa Habari, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema falsafa ya 4R ya Rais Samia imefungua kwa kiasi kikubwa uhuru wa vyombo vya habari nchini. Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Susan Namondo, aliyeipongeza Tanzania kwa mageuzi ya sheria za habari na uhalifu wa mtandaoni.
Katika maadhimisho hayo, MCT ilitoa tuzo maalum za heshima kwa marais wastaafu waliofariki: Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa mchango wake katika kutumia vyombo vya habari kwa ukombozi, na Hayati Ali Hassan Mwinyi, kwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi na uhuru wa habari uliozaa taasisi kama MCT.