MCT Yatimiza Miaka 30: Safari Ndefu ya Kupigania Uhuru wa Habari Tanzania

it | Tue Jul 22 2025


MCT Yatimiza Miaka 30: Safari Ndefu ya Kupigania Uhuru wa Habari Tanzania

Baraza la Habari Tanzania (MCT) linaadhimisha miaka thelathini tangu kuanzishwa kwake Juni 30, 1995. Lilizaliwa kutokana na juhudi za wadau huru wa vyombo vya habari, likiwa na lengo kuu la kutoa jukwaa huru la kutatua migogoro inayotokana na ripoti za habari na kusimamia maadili ya taaluma hii muhimu bila kutegemea mfumo rasmi wa mahakama.


Awali, wadau waliona umuhimu wa kuwa na chombo chao cha kusuluhisha mizozo ya kimaadili na kitaaluma bila kulazimika kufika mahakamani. Baada ya kusajiliwa rasmi na Msajili wa Taasisi mwaka 1997, MCT ilianza shughuli zake kikamilifu. Mbali na usuluhishi na kutoa mafunzo mbalimbali kwa waandishi wa habari, MCT pia ilijikita katika mapambano ya kurekebisha sheria mbalimbali zinazohusu tasnia ya habari.


Juhudi hizi zimefanywa chini ya mwavuli wa Umoja wa Wadau wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), ambao ni muungano wa hiari unaojumuisha asasi zisizo za kiserikali. Wanachama wa CoRI ni pamoja na MCT yenyewe, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Ushirikiano huu umekuwa nguzo muhimu katika mafanikio mengi ya MCT katika kipindi chote cha miaka 30.


Moja ya mafanikio makubwa ya MCT na CoRI ni mchango wao mkubwa katika mchakato wa mageuzi ya sheria za habari, ulioanza rasmi mwaka 2006. Ikumbukwe, mwaka 1993, serikali iliwahi kuandaa muswada uliopendekezwa uitwao "Media Profession Regulation Bill", ambao ulipingwa vikali na wadau wa habari. Sababu ilikuwa ni hofu kwamba muswada huo ungefifisha uhuru wa vyombo vya habari na kuhatarisha uhuru wa kujieleza. Umoja wa wadau uliibuka kupinga muswada huo, na hii iliweka msingi wa ushirikiano wa baadaye.


Mwaka 2006, mikutano kadhaa ilifanyika, ikiongozwa na MISA-TAN, TAMWA, na MCT, ambazo ziliunda CoRI. Lengo lilikuwa kujadili hitaji la sheria mpya na umuhimu wa maoni ya wadau. Iliazimiwa kukusanya maoni kutoka kote nchini, mchakato ulioratibiwa na MCT. Wakati huo, mjadala mkubwa uliibuka kuhusu ikiwa kunapaswa kuwepo sheria moja au mbili zinazosimamia habari. Serikali ilitaka sheria moja, lakini wadau walisisitiza sheria mbili: moja ya Haki ya Kupata Taarifa (kwa kila mtu) na nyingine ya Huduma za Vyombo vya Habari (kwa ajili ya kusimamia vyombo vya habari na wanataaluma).


Kufuatia mijadala hiyo, mwaka 2007 MCT na washirika wake walichapisha muswada mbadala wa wadau kuhusu Haki ya Kupata Taarifa, uliotokana na maoni yaliyokusanywa. Mwaka uliofuata, 2008, walichapisha muswada mbadala wa wadau wa Huduma za Vyombo vya Habari. Utafiti na uandaaji wa miswada hii uliongozwa na marehemu Dk. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akishirikiana na wakili Mohammed Tibanyendera na Dk. Damas Ndumbaro, ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria. Miswada hii iliwasilishwa serikalini kwa matumaini kuwa maoni ya wadau yangezingatiwa. Juhudi hizi zote zililenga kuepuka sheria zenye sura ya udhibiti, kama ilivyokuwa na Sheria ya Magazeti ya 1976.


Ili kuhakikisha upatikanaji wa sheria bora zaidi, mwaka 2011 CoRI kupitia MCT iliandaa safari ya mafunzo kwa wabunge kwenda India mwaka 2012. Lengo lilikuwa kujifunza jinsi nchi zenye sheria nzuri za habari na haki ya kupata taarifa zinavyofanya kazi. Ujumbe wa wabunge nane, wakiwemo Juma Nkamia, Hussein Mzee, Assumpter Mshama, Rebecca Mngodo, Jussa Ismail Ladhu, Ali Mzee, Ramadhani Saleh na Moza Abeid Saidy, ulisafiri kwa wiki moja.


Baada ya miaka kumi ya mapambano, hatimaye Sheria ya Habari ilitungwa mwaka 2016. Hata hivyo, MCT kupitia CoRI iliendelea kufanya vikao na Wizara ya Habari na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, wakiwasilisha mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya Sheria ya Huduma za Habari na ile ya Haki ya Kupata Taarifa. Kati ya mapendekezo 62 waliyopeleka kwenye muswada wa Huduma za Habari, ni 12 tu ndiyo yalichukuliwa kikamilifu, ikiwemo jina la "Huduma za Habari." Mapendekezo 15 yalipokelewa kwa kiasi kidogo, na 35 hayakuzingatiwa kabisa. Hii ni pamoja na mapendekezo muhimu ya kupunguza mamlaka makubwa ya Waziri wa Habari ya kufuta au kufungia vyombo vya habari bila kuwasikiliza wahusika.


Mafanikio mengine ya hivi karibuni ni ushiriki wa MCT na CoRI katika mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya Februari 2023. Serikali iliwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali bungeni, uliokuwa na mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Huduma ya Habari (MSA). MCT na CoRI waliwasilisha mapendekezo takribani 25, wakilenga mamlaka ya Waziri wa Habari ya kufungia magazeti, usajili wa magazeti wa kila mwaka, vifungu vya uchochezi vinavyominya uhuru wa waandishi, pamoja na kutambua makosa ya kashfa kama jinai na uwezo wa polisi kuvamia vyombo vya habari. Walipinga pia adhabu zisizo na ukomo wa juu.


Mabadiliko yaliyopitishwa na Bunge Juni 2023 yalikuwa na ahueni kidogo, kwani vifungu tisa pekee ndivyo vilivyobadilishwa. Hizi ni pamoja na kuondoa mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuratibu matangazo, kuondoa jinai na kuwa madai katika masuala ya kashfa, kuondoa mamlaka ya mahakama kukamata vifaa vya uchapishaji, na kupunguza miaka ya adhabu zinazotokana na ukiukaji wa sheria hii.


Safari ya MCT na CoRI ya kufikia sheria bora za habari bado inaendelea. Wadau wanaendelea kuhamasisha serikali kufanya marekebisho zaidi, hasa kwenye vifungu takribani 12 vya Sheria ya Huduma za Habari ambavyo bado vina utata mkubwa na vinaweza kuhatarisha uhuru wa habari. Mojawapo ni kifungu cha 7(2)(b)(iv), kinachovilazimisha vyombo vya habari binafsi kutangaza taarifa za maslahi ya nchi kwa maelekezo ya serikali. MCT na CoRI wataendelea kushirikiana kuhakikisha kuwa baada ya uchaguzi mkuu ujao, mapendekezo yaliyosalia yanawasilishwa kwa serikali mpya na Bunge jipya ili kufikia sheria kamili ya Huduma za Habari.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.