Rostam Aziz Atema Cheche: 'Vita Sasa ni Mtandaoni, Silaha ni Algorithms, Sio Bunduki'

politics | Tue Jul 15 2025


Rostam Aziz Atema Cheche: 'Vita Sasa ni Mtandaoni, Silaha ni Algorithms, Sio Bunduki'

Mfanyabiashara na mwanasiasa mkongwe, Rostam Aziz, ametoa onyo kali kuhusu usalama wa habari na utambulisho wa Taifa, akisema Tanzania ipo katika vita mpya isiyo ya kawaida—vita inayopiganwa mtandaoni ambapo silaha zake si bunduki, bali ni "algorithms" za mitandao ya kijamii.


Akizungumza leo, Julai 15, 2025, katika mkutano wa pili wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) na Maadhimisho ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Rostam alisema changamoto kubwa inayokabili nchi kwa sasa ni mijadala mingi kuhusu Tanzania kuongozwa na maudhui yanayozalishwa kutoka nje ya nchi.


Alifafanua kuwa maudhui hayo yanatengenezwa na watu wasiofungwa na sheria, mila, wala misingi ya jamii ya Kitanzania. "Watu hawa mara nyingi hawana hisa katika amani yetu, hawana uwekezaji katika maendeleo yetu, na hawawajibiki kwa madhara ya maneno yao. Hii ni hatari kwa roho ya taifa letu," alisema Rostam.


Alisema anaamini kuwa "roho ya taifa inaweza kujengwa au kubomolewa na uadilifu wa mazingira ya habari."


Katika hotuba yake iliyosisimua, alichambua zama hizi mpya za kidijitali, ambapo matumizi ya Akili Mnemba (AI) na mitandao ya kijamii yametawala.


"Tunaishi katika zama ambapo kila simu ya mkononi imekuwa kipaza sauti. Kila ‘like’ au ‘share’ ni kura ya maoni. Na kila uongo usiopingwa, hatimaye huwa sehemu ya kumbukumbu ya taifa," alionya.


Licha ya changamoto hizo, Rostam aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, akisema uhuru katika sekta ya habari umeimarika, weledi unastawi, na wajibu umezingatiwa.


Hotuba ya Rostam Aziz imetafsiriwa kama wito kwa vyombo vya habari vya ndani, wadau wa TEHAMA, na Watanzania kwa ujumla kuwa makini na kulinda anga la habari la nchi dhidi ya upotoshaji na maudhui yenye lengo la kudhoofisha misingi ya taifa.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.