Akiwa katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, eneo lenye historia ndefu ya mivutano ya ardhi, Mgombea Urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ametoa ahadi kabambe ya kutokomeza kabisa migogoro kati ya wakulima na wafugaji ndani ya siku 100 za kwanza za utawala wake endapo atashinda uchaguzi.
Akizungumza na wananchi leo, Ijumaa, Oktoba 3, 2025, katika mkutano wa kampeni, Mwalimu alieleza kuwa tatizo hili sugu limekuwa likiendelezwa na watu wachache wanaolitumia kama mradi wa kujinufaisha kiuchumi na kisiasa, huku wananchi wa kawaida wakiumia. Alisema serikali yake haitavumilia hali hiyo, akiahidi suluhu ya haraka na ya kudumu.
"Ndugu zangu wa Kilosa, hii mivutano ya ardhi si changamoto ya kawaida, hii ni miradi ya watu. Wapo wanaoigeuza kuwa chanzo chao cha mapato na ndiyo maana haiishi. Sisi CHAUMMA, tumeweka kwenye ilani yetu bayana, tukishika tu nchi, ndani ya siku mia moja, kero hii itakuwa historia," alisema Mwalimu kwa msisitizo.
Alikosoa jinsi suala hilo linavyoshughulikiwa sasa, akidai kuwa viongozi wamekuwa wakifika kwa wananchi na kutoa ahadi zisizotekelezeka bila kuonyesha hatua madhubuti za kumaliza tatizo. Alisisitiza kuwa wakulima na wafugaji wote ni Watanzania na wanastahili kuishi kwa amani na usalama, akiahidi kuwa serikali ya CHAUMMA italipa suala hili kipaumbele cha juu zaidi ili kurejesha utulivu na kuwezesha shughuli za uzalishaji mali kuendelea bila vikwazo.