Ahadi za mageuzi makubwa katika sekta ya afya zilizotolewa na mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimepokelewa kwa hisia na matumaini makubwa kote nchini. Wananchi wengi wamezitaja ahadi hizo, hasa inayolenga kukataza tabia ya hospitali kushikilia miili ya marehemu kutokana na madeni, kama hatua ya kihistoria inayogusa utu.
Wakati akizindua kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Dkt. Samia aliahidi kuwa ndani ya siku 100 za kwanza za serikali yake mpya, atahakikisha hakuna hospitali, iwe ya serikali au binafsi, itakayoruhusiwa kuzuia mwili wa marehemu kwa sababu za deni. "Hili jambo linaumiza familia mara mbili; maumivu ya msiba na maumivu ya kushindwa kumstiri mpendwa wao. Tutaunda mfumo mwingine wa kulipia madeni, lakini si kwa kuwageuza marehemu dhamana," alisisitiza Dkt. Samia.
Kauli hii imepongezwa vikali na wananchi, kama anavyosema Mabula Mabula, mkazi wa Dar es Salaam: "Kugusa suala la miili kuzuiwa ni kuonyesha uongozi wenye huruma unaosikiliza vilio vya wanyonge. Ni ahadi inayorejesha heshima na utu."
Zaidi ya hapo, Dkt. Samia alitangaza mapinduzi mengine makubwa, ikiwemo uzinduzi wa Bima ya Afya kwa Wote. Alieleza kuwa awamu ya kwanza italenga makundi maalum kama wazee, watoto, wajawazito, na watu wenye ulemavu, ambao wataingizwa moja kwa moja kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa gharama za serikali.
Sambamba na hilo, aliahidi kuwa serikali itagharamia matibabu ya magonjwa sugu na ya gharama kubwa kwa asilimia 100 kwa wananchi wasio na uwezo. Magonjwa kama saratani, figo, moyo, na kisukari, ambayo yamekuwa yakifilisi familia nyingi, yatatibiwa bure. "Huu ni ukombozi mkubwa, hasa kwa wanawake na familia maskini. Tumekuwa tukishuhudia ndugu zetu wakipoteza maisha kwa kukosa fedha za matibabu," alisema Rebecca Paschal, mkazi wa Arusha.
Ili kutekeleza maono haya, Dkt. Samia ameahidi kuajiri watumishi wa afya wapya 5,000, wakiwemo madaktari na wauguzi, ndani ya siku 100. Hatua hii imepongezwa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Mugisha Nkoronko, aliyesema itasaidia kupunguza upungufu wa watumishi unaokadiriwa kufikia asilimia 60 nchini.
Ahadi hizi zinatolewa wakati mgombea huyo akiendelea na kampeni zake mikoani, ambapo anatarajiwa kuzuru Songwe na Mbeya. Huko, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wana imani na ahadi hizo kutokana na mafanikio yaliyopatikana tayari, kama vile mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri iliyowaokoa kutoka kwa wakopeshaji kandamizi maarufu kama "kausha damu," pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, maji na vituo vya afya.