Chama Cha NCCR-Mageuzi kimetangaza msimamo wake wa kupinga vikali aina yoyote ya maandamano yenye nia ya kuvuruga amani na kuleta taharuki nchini, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29. Chama hicho kimetoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Oktoba 27, 2025, katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Dk. Evaline Munisi, alisisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi muhimu kwa maendeleo.
Dk. Munisi alibainisha kwamba katika Ilani yao ya mwaka 2025, ajenda yao namba moja kati ya ajenda kumi ni Muafaka wa Kitaifa. Alisema muafaka huu unalenga kuleta Maridhiano nchini, kwani chama kinaamini amani na mshikamano wa kweli huletwa na makubaliano ya pamoja. "Tutapata haki na usawa kama ilivyokuwa kwenye kubadili baadhi ya sheria na kanuni za uchaguzi, kwa pamoja vyama vya siasa vilishikamana na kupendekeza marekebisho kwakuwa Serikali ni sikivu," alisema Munisi. Kauli yake inasisitiza nguvu ya mazungumzo na ushirikishwaji wa vyama.
Aidha, chama hicho kilitoa pongezi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi, kwa jinsi anavyosimamia na kutoa malezi mazuri kwa vyama vya siasa. Dk. Munisi alisema malezi hayo yamesababisha kampeni za mwaka huu kuwa tofauti na zilizopita, zikiendeshwa kwa diplomasia ambapo kila mgombea ananadi ilani yake bila magomvi wala kulumbana baina ya vyama.
Pia, NCCR-Mageuzi ilimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza Serikali vizuri bila kutetereka na kwa kuhakikisha usalama unadumu nchini, licha ya kuwepo kwa misukosuko kadhaa iliyoashiria uvunjifu wa amani.