Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amezindua mkakati mpya wa ushirikishwaji wananchi katika kuleta maendeleo, akiwataka kuanzisha miradi muhimu kwa kujenga hatua za awali za majengo (maboma), huku akiahidi kuwa serikali itaingilia kati na kumalizia ujenzi huo hadi utoe huduma. Mtatiro amesema mfumo huu wa ushirikiano ndio njia ya haraka ya kutatua changamoto za huduma za jamii.
Kauli hiyo imetolewa wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata za Lyamidati, Lyabukande, na Mwakitolyo. Akiwa ameambatana na wataalamu wa Halmashauri, Mtatiro alionesha kufurahishwa kwake na moyo wa kujitolea wa wananchi. Alitoa mfano hai wa Kijiji cha Kizungu katika Kata ya Lyamidati, ambako wananchi wameanza ujenzi wa shule shikizi ya Matogoro.
"Nawapongeza sana wananchi wa Kizungu kwa hatua hii. Huu ndio uzalendo ninaotaka kuuona. Nawahakikishia, pindi ujenzi utakapofika hatua ya kuezeka (renta), serikali itaingia na kumalizia kila kitu ili watoto waanze kusoma," alisema Mtatiro, kauli iliyopokelewa kwa shangwe.
Ili kuthibitisha ahadi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mwita Waryuba, alitangaza papo hapo kuwa serikali itatoa Shilingi milioni 5 ili kuendeleza ujenzi huo mara moja.
Wakati wa mikutano hiyo, wananchi walipata fursa ya kueleza changamoto nyingine zinazowakabili, zikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, uhaba wa maji safi na salama, ukosefu wa umeme, upungufu wa watumishi wa afya, pamoja na tatizo la mtandao wa simu.
Akijibu kuhusu upungufu wa watumishi, Waryuba alikiri kuwa ni changamoto ya kitaifa lakini aliahidi kuwa ajira mpya zitakapotoka, mgao utafanywa kwa usawa. Aliongeza kuwa kero nyingi zilizowasilishwa tayari ziko kwenye mipango ya bajeti na zitatekelezwa kama alivyoagiza Mkuu wa Wilaya.
Ili kuhakikisha uwajibikaji, Mtatiro amewaagiza wataalamu wote walioambatana naye kuandaa mrejesho wa maandishi unaoonyesha jinsi kila kero itakavyoshughulikiwa na lini itapatiwa ufumbuzi.