Mgombea urais anayewakilisha Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, amewasha moto wa matumaini katika mji wa Kahama, akiahidi kuleta mapinduzi ya kiuchumi endapo atachaguliwa kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu ujao. Akizungumza na umati mkubwa wa wananchi na wafanyabiashara katika eneo la soko la sasa la CDT, Doyo alieleza kusikitishwa kwake na hali duni ya miundombinu ya biashara, akiahidi ujenzi wa soko jipya la kisasa litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wote.
Alisema ni aibu kuona wafanyabiashara, ambao ni injini ya uchumi, wakifanya kazi zao katika mazingira yasiyo rasmi na yasiyo na huduma muhimu. "Serikali ya NLD itahakikisha inajenga soko la hadhi ya juu hapa Kahama. Soko lenye sakafu safi, umeme wa uhakika na maji safi na salama. Tunataka mfanye biashara zenu kwa heshima na ufanisi, siyo kwa kubahatisha," alisisitiza Doyo huku akishangiliwa.
Mgombea huyo aligusia kwa kina kitendawili cha Mkoa wa Shinyanga, hasa Wilaya ya Kahama, kuwa eneo lenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu lakini wakazi wake wengi wakiendelea kuogelea katika lindi la umaskini. "Hii haiwezekani na haikubaliki. Neema ya madini yaliyopo chini ya ardhi yenu lazima iwanufaishe ninyi kwanza kabla ya mtu mwingine. Tutaunda mfumo utakaohakikisha mapato ya rasilimali hizi yanabaki hapa na kuinua maisha ya kila mwananchi," aliahidi.
Doyo alifafanua kuwa dira ya serikali yake ni kujenga taifa lenye usawa, haki na maendeleo yanayomgusa kila mtu. Alisema anataka kuona Watanzania wakiwa huru, wenye elimu na fursa sawa za kushiriki katika ujenzi wa taifa lao. Aliahidi kuwa serikali yake itakuwa sikivu, itakayoweka kipaumbele katika kutatua kero za wananchi kwenye sekta za afya, ajira, kilimo, viwanda na miundombinu ili kujenga uchumi imara na shirikishi.