Katika kile kinachoonekana kama "kutwanga maji kwenye kinu," Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) katika Wilaya ya Shinyanga yameinua sauti zao dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yakilalamikia kubebeshwa mzigo mzito wa kodi zinazofanana na zile zinazotozwa makampuni ya kibiashara yenye lengo la kupata faida, huku yenyewe yakijikita katika kutoa huduma za kijamii.
Sakata hilo limeibuka kwa kishindo leo, Desemba 12, 2025, katika kikao muhimu cha Robo ya Nne ya Mwaka (Septemba-Desemba) cha Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGo) wilayani humo. Akisoma risala nzito mbele ya meza kuu, Mwenyekiti wa NaCoNGo Wilaya ya Shinyanga, Bw. Lucas Maganga, ameweka bayana kuwa licha ya nia njema ya serikali, bado kuna "miba" inayochoma utendaji wao.
"Tunashukuru serikali kwa kututua mizigo mingi ya urasimu huko nyuma, lakini bado kuna 'mfupa ulioshindikana'. Tunatozwa kodi kubwa utadhani sisi ni wafanyabiashara wa maduka, ilhali sisi ni wadau wa maendeleo," alieleza Maganga kwa masikitiko.
Kiini cha malalamiko hayo ni ugumu na urasimu uliokithiri katika kupata Hadhi ya Hisani (Charitable Status) kutoka TRA, hadhi ambayo huwapa nafuu ya kodi. Maganga amependekeza dawa ya changamoto hii ni TRA kufanya mapitio ya haraka ya miongozo yake ili kuweka mstari mwekundu unaotenganisha miradi ya kijamii na ile ya kibiashara.
"Tunapendekeza kuwepo kwa dirisha maalum au 'dawati la NGOs' katika ofisi za TRA ngazi ya wilaya na mkoa. Hii itasaidia kuondoa msongamano na kuweka utaratibu wa 'One Stop Center' ili vibali na misamaha ya kodi ipatikane bila kuzungushwa mbuyu," alisisitiza kiongozi huyo.
Akijibu hoja hizo nzito, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, alionyesha ukomavu wa kiuongozi kwa kukiri kuzipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi. Mtatiro, anayefahamika kwa misimamo yake thabiti, aliwashauri viongozi hao kuanzisha mawasiliano rasmi kisheria (Official Communication) ili hoja zao zipate mashiko kiserikali.
Hata hivyo, DC Mtatiro hakusita "kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa" wale wanaolegalega. Alitoa angalizo kali kwa mashirika ambayo yapo "mfukoni" (briefcase NGOs) na yasiyo na tija kwa wananchi wa Shinyanga.
"Serikali inawathamini sana kama wabia wetu wa maendeleo, lakini lazima twende na wakati. Mashirika yasiyo na tija, yale ambayo yapo tu kwenye makaratasi, yajiandae kufutwa. Tunataka kuona matokeo yanayogusa maisha ya mwananchi wa kawaida, siyo ripoti za mezani tu," alionya Mtatiro.
Katika kuwapa mwanga wa kulekea mwaka 2026, DC Mtatiro ameyataka mashirika hayo kubadili upepo na kuanza kuandika maandiko ya miradi inayolenga Amani, Usalama, Utengamano na Ushauri kwa Vijana. Alibainisha kuwa maeneo hayo ndiyo "keki ya taifa" ilipo kwa sasa, ikizingatiwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda Wizara maalum ya Vijana na wafadhili wengi wameelekeza nguvu huko.
Shinyanga, mkoa unaosifika kwa utajiri wa madini na kilimo cha pamba, unategemea sana NGOs kuziba mapengo katika sekta ya afya, elimu, na ustawi wa jamii. Wito wa NaCoNGo ni kuhakikisha kuwa fedha zinazopatikana zinaenda kuhudumia wananchi badala ya kurejeshwa serikalini kama kodi, jambo ambalo linaonekana kama kuhamisha fedha kutoka mfuko wa kushoto kwenda wa kulia bila tija ya moja kwa moja kwa walengwa.