Mpina Ataka Adhabu ya Kunyongwa kwa Wabadhirifu wa Mali ya Umma

politics | Fri Mar 07 2025


Mpina Ataka Adhabu ya Kunyongwa kwa Wabadhirifu wa Mali ya Umma

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina, ametoa wito kwa serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia na kupitisha sheria kali dhidi ya ubadhirifu wa mali za umma, ikiwemo adhabu ya kunyongwa kwa wahusika. Kauli hii imekuja baada ya Mbunge wa Mbogwe, Nicodemas Maganga, kuwasilisha hoja bungeni akiwataka wabunge kuunga mkono sheria itakayotoa adhabu ya kunyongwa kwa wezi, mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu wa fedha za umma.


Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakafuru, Halmashauri ya Mbogwe, Mpina alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya kodi za wananchi yanakwamisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii na kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Aliongeza kuwa kutokana na mafisadi wachache, wananchi bado wanakabiliwa na vifo vya wajawazito na watoto, wagonjwa kukosa huduma muhimu hospitalini, na elimu duni kutokana na ukosefu wa miundombinu bora.


"Fedha za umma zikitumiwa vibaya, hospitali zitakosa dawa na madaktari wa kutosha. Watu wangapi wamepoteza maisha kwa kukosa huduma hizo muhimu? Watoto wangapi wamefariki kwa kukosa damu kwa sababu fedha zinaliwa na mafisadi?" alihoji Mpina.


Mbunge huyo alieleza kuwa alipoandikisha jina lake kuunga mkono hoja hiyo bungeni, alikuwa wa 121, na hadi sasa wabunge 168 wamekubali pendekezo hilo. Aliongeza kuwa hoja hiyo itajadiliwa kwa kina katika Bunge lijalo la bajeti ili kuona iwapo adhabu kali inaweza kusaidia kudhibiti ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.


Mpina pia alibainisha kuwa alipowasilisha mchango wake kwenye tume ya maboresho ya kodi, aliandika ripoti yenye kurasa 235, iliyobaini kuwa takribani shilingi trilioni 42 hupotea kila mwaka kutokana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.


Awali, Mbunge wa Mbogwe, Nicodemas Maganga, alieleza kuwa serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 74 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara. Alisisitiza kuwa fedha hizo zinalenga kuboresha huduma za jamii na kuinua maisha ya wananchi.


Maganga pia aliongeza kuwa hakuna mwekezaji wa kigeni, hususan kutoka China, atakayeruhusiwa kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa wachimbaji wadogo bila utaratibu maalum, akisisitiza kuwa wananchi watapewa kipaumbele kunufaika na rasilimali zao.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.