Msuguano mkali unaotafuna Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umefikia pabaya, baada ya Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam kuingilia kati mgogoro wa ndani unaoweza kuwatia gerezani baadhi ya viongozi wake wakuu. Katika hatua isiyo ya kawaida, Mahakama imewapa siku nane viongozi tisa waandamizi wa chama hicho, akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche na Kaimu Katibu Mkuu John Mnyika, kujibu tuhuma nzito zilizowasilishwa na wenzao kutoka Zanzibar.
Shauri hili, lililofunguliwa kwa hati ya dharura, linatokana na maombi yaliyowasilishwa na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis, Maulida Anna Komu, pamoja na Makamu Mwenyekiti mstaafu Said Issa Mohamed. Wanachama hawa wanaiomba mahakama itoe amri ya kuwakamata na kuwashikilia viongozi hao kama "wafungwa wa madai," kwa madai ya kukaidi na kudharau amri halali iliyotolewa awali na chombo hicho cha sheria.
Kiini cha mzozo huu ni amri ya mahakama ya tarehe Juni 10, 2025, iliyowazuia viongozi hao kujihusisha na shughuli zozote za kisiasa kwa niaba ya chama hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa. Hata hivyo, walalamikaji wanadai kuwa Heche, Mnyika na wenzao saba wamepuuza agizo hilo kwa kuendelea kuendesha mikutano ya waandishi wa habari, vikao vya ndani, na kutoa hotuba mbalimbali, vitendo ambavyo vinadaiwa kulenga kuvuruga maslahi ya shauri kuu lililopo mahakamani.
Mbele ya Jaji Awamu Mbagwa, imeelezwa kuwa viongozi hao wanapaswa kuwasilisha majibu yao kupitia kiapo kinzani ifikapo Oktoba 21, 2025, na shauri lenyewe litasikilizwa rasmi siku inayofuata. Hatima ya viongozi hawa sasa ipo mikononi mwa mahakama, katika kesi inayoanika wazi mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani, unaohusishwa na masuala ya uongozi pamoja na mgawanyo wa rasilimali ndani ya muundo wa chama hicho, hasa upande wa Zanzibar.