Viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamemaliza mfululizo wa mikutano minane ya hadhara katika Mkoa wa Morogoro, wakisisitiza kauli yao maarufu ya 'Hakuna Matengenezo, Hakuna Uchaguzi'. Lengo kuu la mikutano hii lilikuwa ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa misingi ya demokrasia na utawala bora, huku wakirejea falsafa za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Msafara wa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, ulianzia maeneo ya Mwaya (Kilombero), kisha ukaendelea Ruaha na Mikumi Mjini (Mikumi). Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alianzia Wilayani Kilosa, akifanya mikutano katika maeneo ya Dumila, Mvumi, na Kimamba. Mikutano yote hii ilihitimishwa kwa mkutano mkubwa wa pamoja mjini Morogoro, ambapo mamia ya wananchi walijitokeza kusikiliza ujumbe wa viongozi hao.
Katika hotuba zake, John Heche alikumbushia maneno ya Mwalimu Nyerere kuhusu nguzo nne muhimu zinazochochea maendeleo ya taifa: watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora. Alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na watu wenye vipaji na utaalamu wa kila aina, pamoja na ardhi pana yenye rasilimali nyingi kama vile madini, misitu, udongo wenye rutuba, mito, na maziwa. Hata hivyo, Heche alidai kuwa kikwazo kikuu cha maendeleo nchini kwa sasa ni kukosekana kwa siasa safi na uongozi bora.
Heche alikishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kueneza siasa za propaganda ambazo zimechangia udanganyifu mkubwa wakati wa chaguzi, ikiwemo kuondoa wagombea wa vyama vya upinzani kwa visingizio mbalimbali. Alitoa mfano wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika mwaka jana, ambapo wagombea wengi wa upinzani waliondolewa kwa madai ya kutokujua kusoma na kuandika, madai ambayo aliyasema hayakuwa na ukweli wowote.
"Nchi hii imetawaliwa na siasa chafu, zilizojikita kwenye rushwa na hata mauaji. Mnachagua watu wanakataliwa bila sababu za msingi. Ndio maana tumesema hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi katika mazingira haya," Heche alifafanua akisisitiza msimamo wa CHADEMA. Aliongeza kuwa Katiba ya nchi inaeleza wazi kuwa serikali inapaswa kufanya kazi kwa lengo la ustawi wa wananchi na kuwajibika kwao, huku ikipata mamlaka yake kutoka kwao kupitia chaguzi huru na haki.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika, alitumia mikutano yake kutoa elimu ya Katiba na sheria za uchaguzi kwa wananchi wa Morogoro. Alirejea matukio ya kusikitisha ya uchaguzi uliopita, akibainisha kuwa baadhi ya wagombea wa CHADEMA ngazi ya vijiji walipoteza maisha. Mnyika alionya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu endapo matengenezo muhimu ya sheria na mfumo wa uchaguzi hayatafanyika. Alimalizia kwa kusema kuwa vitendo vya kuengua wagombea na figisufigisu zilizoshuhudiwa katika chaguzi za serikali za mitaa ni dalili mbaya kwa uchaguzi wa madiwani, wabunge, na rais.