Hali ya kisiasa nchini Tanzania inaonekana kuingia katika sintofahamu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, huku misimamo mikali ya kisiasa ikitishia mshikamano wa kitaifa. Kaulimbiu pinzani kama "Oktoba Tunatiki" kutoka Chama Tawala, "No Reforms, No Election" inayobebwa na baadhi ya vyama vya upinzani, na "Oktoba Linda Kura," zimelazimu Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuingilia kati, likiomba kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwasilisha mapendekezo ya kuunusuru mchakato huo.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, alieleza kuwa chama hicho kina wasiwasi mkubwa kwamba mgawanyiko unaoonekana sasa unaweza kusababisha machafuko na kuvuruga amani wakati na baada ya uchaguzi. Alisema lengo la kutaka kuonana na Rais Samia ni kumshauri kama kiongozi mkuu wa nchi juu ya hatua za dharura zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki, na unaolinda amani ya taifa.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, TLS imetumia miezi minne iliyopita kufanya mashauriano ya kina na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa, na watu wenye ushawishi. Matokeo ya mazungumzo hayo yamebaini kuwepo kwa maeneo 21 muhimu katika kanuni na sheria za uchaguzi ambayo yanahitaji marekebisho ya haraka ili kuondoa hofu na sintofahamu iliyopo.
"Tunaamini maeneo haya 21 yakifanyiwa marekebisho, tutaingia kwenye uchaguzi kama taifa moja na tutatoka tukiwa na mshikamano," alisisitiza Mwabukusi. Alitoa mfano wa dosari iliyopo ambapo sheria inamtaka msimamizi wa uchaguzi kutoa fomu za matokeo kwa mawakala, lakini kanuni zinampa mamlaka ya kuamua kutoa au kutotoa, jambo linaloacha mwanya wa sintofahamu.
TLS inasisitiza kuwa mamlaka ya mwisho ya nchi yapo kwa wananchi kama inavyoelezwa na Ibara ya Nane ya Katiba, na hivyo uchaguzi unapaswa kuwa shughuli ya kiraia na si kumilikishwa na Tume ya Uchaguzi pekee. "Ni jukumu letu kumkumbusha Rais kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote, si Rais wa CCM. Tunataka aone na kusikia kile ambacho wananchi wanazungumza kupitia kwetu," aliongeza.
Pendekezo hili la TLS linaungwa mkono na taasisi zenye uzito nchini, zikiwemo Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), na Shura ya Maimamu. Vilevile, vyama vya siasa wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kama CHADEMA, ACT-Wazalendo, CUF, na NCCR-Mageuzi navyo vimeunga mkono hoja hiyo. Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikuweza kutuma mwakilishi kwenye vikao hivyo kutokana na kuwa katika michakato yake ya ndani ya uchaguzi.
Mbali na marekebisho hayo 21, wadau wote wamependekeza kuundwa kwa kamati maalum shirikishi itakayojumuisha makundi yote ya kijamii ili kusimamia utekelezaji wa hatua za muda mfupi na mrefu za kuhakikisha haki, amani na utawala bora vinadumishwa nchini.