Maumivu Baada ya Uchaguzi: Mkazi wa Gongo la Mboto Apigania Uhai, Aililia Jamii Imokoe

politics | Mon Nov 10 2025


Maumivu Baada ya Uchaguzi: Mkazi wa Gongo la Mboto Apigania Uhai, Aililia Jamii Imokoe

Wakati vumbi la Uchaguzi Mkuu likiwa limetulia na maisha ya wengi yakirejea katika hali ya kawaida, hali ni tofauti kabisa kwa Bw. Salum Mlyatangu, mkazi wa eneo la Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam. Kwake yeye, siku ya uchaguzi imebaki kuwa kovu lisilofutika, baada ya kujikuta katikati ya purukushani zilizomwacha na majeraha mabaya yanayotishia ustawi wa maisha yake.


Bw. Mlyatangu alikumbwa na mkasa huu mzito akiwa katika eneo lake la kujitafutia riziki. Katika kile kinachoonekana kama ajali ya kuwa mahali pasipo sahihi kwa wakati usio sahihi, alijeruhiwa vibaya na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu la kutoa machozi au 'stani' lililorushwa na askari waliokuwa katika harakati za kutuliza ghasia za waandamanaji zilizozuka siku hiyo.


Athari za tukio hilo zimemwacha Bw. Mlyatangu katika hali ngumu ya kiafya. Ameapata majeraha makubwa maeneo nyeti ya mwili wake ikiwemo tumboni, kwapani, na mkononi. Majeraha haya yamemfanya asiweze tena kujishughulisha, jambo ambalo ni pigo kubwa kwake na familia inayomtegemea, hasa ukizingatia hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa kawaida anayenitegemea kipato cha siku.


Familia yake sasa imelemewa na mzigo wa gharama za matibabu. Dada wa majeruhi huyo, Bi. Hajira Sagamiko, amepaza sauti kwa niaba ya familia, akiwaomba Watanzania wenye moyo wa huruma na serikali kuwatazama kwa jicho la 'utu'.


"Hali ya kaka yetu inazidi kuwa mbaya siku hadi siku," anasimulia Bi. Hajira kwa uchungu. "Anahitaji vipimo zaidi, kama vile X-ray, ili madaktari waweze kuona ukubwa wa tatizo kwa ndani, lakini tumekwama kutokana na ukata. Hawezi kutembea vizuri, na maumivu ni makali mno licha ya kushonwa nyuzi kadhaa tumboni na kwapani. Kama familia, tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu, lakini sasa tumefika ukomo, tunahitaji nguvu ya ziada kuokoa uhai wake."


Kilio cha Bw. Mlyatangu ni kielelezo cha uhalisia unaowakabili baadhi ya wananchi wanaojikuta wahanga wa matukio yasiyotarajiwa. Kwa sasa, anahitaji zaidi ya pole; anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kupata matibabu stahiki na kurejea katika hali yake ya kawaida aweze kuendelea na ujenzi wa taifa.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.