Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amewatoa hofu wananchi wa wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, kwa kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwaletea maendeleo endelevu. Aidha, amewaahidi wanaoishi katika visiwa vilivyoko ndani ya wilaya hiyo kuwa serikali itaendelea kuboresha vyombo vya usafiri ili kuhakikisha usalama wao unakuwa wa uhakika.
Makalla aliyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Muleba, akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya siku saba. Katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa usalama kwa wakazi wa visiwa, akibainisha kuwa serikali inatambua changamoto wanazokabiliana nazo katika usafiri na itaendelea kuwekeza katika maboresho.
“Tunaahidi tutaendelea kushirikiana nanyi kwa karibu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuwaletea maendeleo yanayolenga kuboresha maisha yenu. Imani kubwa mliyonayo kwa CCM inatokana na dhamana tuliyopewa na wananchi, na tutaendelea kuheshimu na kutekeleza wajibu huo,” alisema Makalla kwa msisitizo.
Alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameiweka Muleba katika ramani ya maendeleo kwa kuwekeza katika miradi muhimu ya afya na maji ambayo tayari inatekelezwa. Alitaja mradi mkubwa wa maji wa kimkakati wenye thamani ya shilingi bilioni 39, ambao utahusisha uchotaji maji kutoka Ziwa Victoria na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Alifafanua kuwa mradi huu utakapokamilika, utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wengi wa Muleba.
Katika kuelekea kipindi cha uchaguzi, Makalla aliwataka wananchi kuwa makini na wale wanaojaribu kuwapotosha kwa kejeli na propaganda za uongo dhidi ya CCM. Aliwashauri wananchi kuachana na watu kama hao na badala yake kuendelea kukiamini na kukichagua CCM, ambacho amesisitiza kuwa ndicho chama pekee kinachojali maslahi yao na kuwaletea maendeleo halisi.