Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeahidi kuendeleza amani na utulivu nchini chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo bila vikwazo. Chama hicho kimewataka wananchi kuwa makini na watu wenye hila na mipango ya uchochezi, na kuwakataa wale wanaotaka kuwagawa.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, aliyasema haya leo wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Katoro, mkoani Geita, katika mkutano wa hadhara, akiwa katika ziara yake ya siku saba inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, na Simiyu. Makalla alimsifu Rais Samia kama mzalendo na mwadilifu, akisisitiza kuwa usimamizi wake makini wa rasilimali za nchi ndio unaowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Kama kuna Mtanzania anayebeza maendeleo tuliyopata, kama kuna gari la wagonjwa, basi akimbizwe Hospitali ya Milembe. Mengi yamefanyika, tunakushukuru. Ili tuendelee kupata maendeleo, tudumishe amani,” Makalla aliwaambia Watanzania. Alisisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye amani, na kwamba ushindi wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji ni deni kubwa linalowataka waendelee kuwa karibu na wananchi, kutatua kero zao, na kuwaletea maendeleo.
Akizungumzia wachimbaji wadogo, Makalla alisema azma ya serikali ni kuwajali, akiongeza kuwa wachimbaji wakubwa walianza kama wadogo. “Azma ya chama ni kuhakikisha tunawajali wachimbaji wadogo. Wakipewa fursa, wadogo watakua. Hivyo, azma ya CCM ni kuwajali wachimbaji wadogo, wa kati, na wakubwa,” alisema.
Makalla alieleza kuwa Mkoa wa Geita una utajiri wa madini, na kwamba chini ya uongozi wa Rais Samia, miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa. “Hapa wanaleta mradi wa maji wa shilingi bilioni sita, barabara, na huduma za afya,” alisema. Aliongeza kuwa walipofika Katoro, walishuhudia shida kubwa ya maji, lakini chini ya Rais Samia, kero hiyo inakwenda kuisha. Aidha, shilingi milioni 800 zimetolewa ili kuongeza usambazaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
“Ilikuwa ukipita hapa usiku ni giza, lakini Rais Samia ameleta fedha kuweka taa 170 katika mji wenu. Kuna hospitali, barabara. Tunaamini kwamba miradi ya maendeleo imekuwa sehemu ya kushawishi wananchi kukiamini CCM,” alisema Makalla.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, alithibitisha kuwa Rais Samia alipopita Katoro Oktoba 15, 2022, aliahidi kuweka taa barabarani, na ahadi hiyo imetekelezwa. Taa hizo zinawawezesha wafanyabiashara kufanya kazi hadi usiku. Shigella aliongeza kuwa ujenzi wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita mbili umeanza, na mipango ipo ya kuongeza hadi kilomita tano. Alitoa ombi kwa Makalla kuendeleza juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi wa Katoro.