Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewataka wanachama wa chama hicho kujiandaa kwa mapambano makali katika harakati zao za kuzuia uchaguzi mkuu ujao. Akizungumza na wanachama wa Chadema wilayani Mbozi, mkoani Songwe, Lissu alisisitiza kuwa mkakati wao wa kuzuia uchaguzi ni hatua kubwa na ya kihistoria katika siasa za Tanzania.
Lissu alieleza kuwa Chadema ndicho chama cha kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992 kuja na mpango wa kuzuia uchaguzi. "Hakuna chama kingine kilichowahi kuthubutu kusema kwamba tutazuia uchaguzi kama hatutakuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi," alisema Lissu.
Aliongeza kuwa kuzuia uchaguzi ni sawa na kupinga ratiba iliyowekwa kisheria na kikatiba ya kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. "Hii ni hatua kubwa sana, na hakuna mtu asiyejua hilo. Ni jambo la kihistoria katika siasa za vyama vingi nchini," alisisitiza Lissu.
Lissu aliwaonya wanachama kuwa harakati hii haitakuwa rahisi na itahitaji ushiriki mkubwa na umoja kutoka kwa wanachama wote. "Tunahitaji kujiandaa vyema kwa mapambano haya. Hii siyo kazi rahisi, lakini tunaamini tunaweza kufanikiwa," aliongeza.
Chadema imekuwa ikishinikiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao, wakidai kuwa mfumo uliopo hauko huru na haki. Msimamo wao wa kuzuia uchaguzi ni ishara ya kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa nchini.