Chama cha National League for Democracy (NLD) kimethibitisha hadharani nia yake ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na kupuuza wito wa baadhi ya vyama vya upinzani wanaotaka mageuzi ya mfumo wa uchaguzi kabla ya kushiriki. Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, alisisitiza kuwa chama chake hakitasusia uchaguzi, bali kitaendelea kuwaeleza wananchi sera zake ili kupata ridhaa ya kuongoza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika Februari 23, 2025, eneo la Buguruni, Ilala jijini Dar es Salaam, Doyo alibainisha kuwa NLD haijaunga mkono msimamo wa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye amekuwa akipinga kushiriki uchaguzi bila mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, akitumia kauli yake maarufu ya "No reforms, no election".
Doyo alieleza kuwa, ingawa NLD kilikuwa miongoni mwa vyama vilivyoathirika na Muungano wa UKAWA mwaka 2015, chama chake hakitakubali kurudia makosa hayo. Alisema kuwa, licha ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na NLD kushirikiana ili kuiondoa CCM madarakani, chama chake kilidhurumiwa kwa wagombea wake kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.
"Tupo vyama 19 vya siasa, ikiwemo NLD. Hatutokimbilia msituni wala kususia uchaguzi. Tunaendelea kuwaeleza wananchi sera zetu ili watupatie ridhaa ya kuwaongoza," alisema Doyo.
Mwenyekiti wa Taifa wa NLD, Mfaume Khamis Hassan, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha walimu wanaojitolea wanapata ajira za kudumu. Aidha, aliwasihi Watanzania kudumisha amani na kuepuka kushabikia siasa zinazoweza kusababisha machafuko nchini.
Katika hatua nyingine, Mfaume alimpongeza Rais Samia kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi ujao, huku akimtakia kila la heri katika safari yake ya kisiasa. Hii inaashiria msimamo wa NLD wa kufanya kazi na serikali iliyopo, huku wakiendelea na harakati zao za kisiasa.