Lipumba: Sera za CUF Zitaleta Haki, Uchumi Bora na Furaha kwa Watanzania

politics | Mon Apr 07 2025


Lipumba: Sera za CUF Zitaleta Haki, Uchumi Bora na Furaha kwa Watanzania

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa chama chake kina sera madhubuti zitakazowawezesha Watanzania kujikomboa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Alieleza kuwa CUF inalenga kujenga nchi ambayo inatoa haki sawa na furaha kwa kila mwananchi.


Akizungumza na umma kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujiunga na CUF na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, ikiwa ni pamoja na udiwani, uwakilishi, ubunge, na urais kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.


Profesa Lipumba alieleza kuwa moja ya sera muhimu za CUF katika kukabiliana na umasikini ni utekelezaji wa hatua kwa hatua wa mpango wa Kipato cha Msingi kwa Wote (Universal Basic Income), akisisitiza kuwa ni haki ya kila Mtanzania kuwa na uhakika wa kipato cha msingi.


Akizungumzia sekta ya afya, Profesa Lipumba alikiri kuwepo kwa mafanikio katika kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 mwaka 2022, na kupungua kwa vifo vya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja kutoka 99 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 1999 hadi 43 mwaka 2022. Hata hivyo, alidai kuwa sera ya serikali ya kutoa matibabu bure kwa wanawake wajawazito, watoto na wazee ni kama danganya toto kwa kuwa uhalisia unaonyesha vinginevyo.


Kuhusu elimu, Profesa Lipumba alielezea hali ngumu inayowakabili wazazi na walezi katika shule za msingi za umma kote nchini. Alisema kuwa wanafunzi wanalazimika kuchangia kati ya Shilingi 800 hadi Shilingi 1,500 kila siku kwa ajili ya michango mbalimbali, hasa katika maeneo ya mijini. Aliongeza kuwa wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kitaifa (darasa la nne na la saba) wanalazimika kuchangia Shilingi 2,000 kila wiki kwa ajili ya mitihani ya mwisho wa wiki, akisema kuwa huu ni mzigo mkubwa kwa wazazi na walezi, hasa wale wenye watoto zaidi ya mmoja shuleni. Alisisitiza kuwa kama elimu inagharamiwa na serikali, basi inapaswa kuwa bure kabisa kwa wazazi.


Kwa ujumla, Profesa Lipumba alieleza kuwa CUF ina dira ya kuleta mabadiliko chanya kwa Watanzania kwa kutekeleza sera zinazolenga kuboresha maisha yao katika nyanja zote, kuanzia siasa, uchumi hadi masuala ya kijamii.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.