LEAT Yatoa Mafunzo Kuhusu Athari za Uchimbaji wa Makaa ya Mawe

politics | Sat Mar 29 2025


LEAT Yatoa Mafunzo Kuhusu Athari za Uchimbaji wa Makaa ya Mawe

Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) kimeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari na wadau wa maendeleo kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu uchimbaji wa makaa ya mawe na athari zake kwa jamii. Mafunzo hayo yamefanyika leo Machi 28, jijini Dar es Salaam.


Ofisa Tathmini kutoka LEAT, Augustino Munuma, alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono kampeni dhidi ya uchimbaji wa makaa ya mawe, kwa kuzingatia afya za wananchi na utunzaji wa mazingira.


“LEAT ni marafiki wa Mazingira Tanzania. Tulifanya utafiti kuhusu uchimbaji wa makaa ya mawe mkoani Ruvuma, na tumebaini kuna changamoto nyingi ambazo zinahitaji kushughulikiwa, ikiwemo suala la utunzaji wa mazingira na kujali afya za wananchi kutokana na vumbi linalotokana na uchimbaji,” alisema Munuma.


Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Deodatus Mfugale, ambaye ni mwandishi wa habari mwandamizi wa masuala ya mazingira, aliwahimiza waandishi wa habari kuandika zaidi habari zinazosaidia jamii badala ya kusifia viongozi kila siku.


Alisema kuwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye rasilimali za madini wanahitaji kunufaika na rasilimali hizo na si kugeuzwa kuwa mateso kwao. Alikiri kuwa uwekezaji ni muhimu kwa sababu unaongeza pato la taifa na kukuza uchumi, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu kwa wawekezaji kufuata sheria za nchi.


Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo walisema kuwa mafunzo hayo yamewajenga katika utekelezaji wa majukumu yao na yatasaidia jamii kunufaika na rasilimali zilizopo bila kuathiri afya zao na kuharibu mazingira.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.