Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewataka viongozi wa bara la Afrika kuwa waaminifu na kuweka maslahi ya bara lao mbele ili kufanikisha malengo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya Waafrika. Alitoa wito huu muhimu wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbeki alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya Afrika yatapatikana tu ikiwa viongozi wataweka mbele maslahi ya nchi zao na kuongoza kwa uadilifu, uwazi, na dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko chanya kwa Waafrika wote. “Tunapoadhimisha Siku ya Afrika mwaka huu kwa kaulimbiu ‘Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia: Kuangazia Historia Yetu, na Kuunda Mustakabali Wetu,’ tunakumbushwa kuwa haki siyo mwisho, bali ni dai endelevu la ukweli, heshima, na uongozi unaoakisi hali halisi za watu wetu. Tunahitaji kuwekeza katika elimu, ubunifu, ushirikishaji wa vijana katika maamuzi, na kupambana na ufisadi ambao unaharibu maendeleo,” alieleza Mbeki.
Aliongeza kuwa Afrika ina utajiri mkubwa na uwezo ambao unahitaji viongozi wenye maono ya mbali, wasioogopa uwajibikaji, na wanaotanguliza maslahi ya wananchi wao na taifa kuliko matakwa yao binafsi. Viongozi ambao wanaweza kufikiria zaidi ya uchaguzi ujao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisisitiza umuhimu wa kila Mwafrika kutafakari mafanikio, changamoto, na matarajio ya kuinua maendeleo ya Afrika kwa amani na utulivu. Alisisitiza pia umuhimu wa kuwaenzi viongozi walioendeleza fikra za Uafrika na wanaopigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa bara la Afrika, kwani wameacha urithi mkubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, tunawakumbuka na kuwapongeza waanzilishi wa Umoja wa Afrika (OAU), ambao ndoto yao ya kuunganisha na kushirikisha zaidi mataifa ya Afrika imeendelea kuishi hadi leo. Tunawaheshimu pia viongozi waliowafuata, ambao waliendeleza dhima ya Uafrika na wanaopigania ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa bara letu,” alisema Balozi Kombo.
Hafla hiyo iliwakutanisha mabalozi, viongozi wa serikali, wastaafu, wanadiplomasia, wasomi, na wawakilishi wa asasi za kiraia na kijamii kusherehekea mshikamano, utofauti, na maendeleo ya Afrika. Usiku huo ulipambwa na burudani za kitamaduni, vyakula kutoka nchi za Afrika, na tafakuri juu ya mchango wa mataifa ya Afrika katika historia na maendeleo ya sasa kuelekea amani na kujitegemea.
Hafla hiyo ilifanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 62 ya Umoja wa Afrika, kuelekea Siku ya Afrika, ambayo huadhimishwa Mei 25 kila mwaka.