Katibu wa CHADEMA katika Jimbo la Iringa, Paschal Chibala, leo ametangaza kuondoka chama chake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tangazo hilo limefanyika katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Katibu wa NEC wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, katika uwanja wa Mwembetogwa, mkoani Iringa.
Chibala alieleza kuwa sababu kuu ya kuhama ni baada ya kubaini kuwa CHADEMA hawana sera madhubuti. Alidai kuwa chama hicho kinawadanganya wananchi kwa ahadi zisizotekelezeka za mageuzi.
Aidha, alitaja tukio lingine lililochangia uamuzi wake, akidai kuwa wakati Mchungaji Peter Msigwa akiwa CHADEMA, alimpelekea mwenyekiti ambaye hakujua kusoma, wakati yeye (Chibala) ana shahada ya elimu.
CPA Amos Makalla alimpokea Chibala na kuwakaribisha wengine wanaotaka kujiunga na CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kina sera zinazowalenga wananchi na maendeleo yao. Mkutano huo ulikuwa sehemu ya hitimisho la ziara ya siku tatu ya CPA Makalla katika mikoa ya Mbeya na Iringa.