Katika mkakati wa kipekee unaolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya taifa, taasisi ya kiraia ya Sauti ya Jamii Kipunguni imeanzisha kampeni ya kuwataka wananchi kuisoma na kuijadili Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025–2050. Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika katika mazingira yasiyo ya kawaida – ndani ya saluni ya kike iliyopo Kipunguni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya kupeleka mijadala ya kitaifa kwenye maeneo wanayokutana wananchi kila siku.
Akizungumza wakati wa mjadala huo, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Fatma Abdurahman, alisema lengo kuu ni kuhakikisha kila Mtanzania anaielewa dira hiyo, ambayo imebeba mustakabali wa maisha yao na mwelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo. Alisema taasisi yao inahimiza mijadala kuhusu dira ifanyike kwenye maeneo yote, kuanzia vijiwe vya kahawa na bodaboda, kwenye vikundi vya vikoba, sokoni, na hata katika nyumba za ibada.
"Tunawashauri wananchi watumie fursa yoyote wanapokutana kujadili na kukumbushana kuhusu Dira ya Taifa. Ni muhimu kuisoma ili kujua kama maoni tuliyotoa wakati wa maandalizi yake yamezingatiwa," alisema Fatma. Aliongeza kuwa kuelewa dira hiyo kutawapa wananchi nguvu ya kuhoji wagombea katika uchaguzi ujao na kupima kama ahadi zao zinaendana na maono ya taifa.
Kampeni hii inakuja wakati muafaka ambapo taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Kwa mujibu wa Sauti ya Jamii Kipunguni, mwananchi anayeielewa Dira ya Maendeleo ana uwezo mkubwa wa kuandaa maswali yenye mashiko kwa wagombea ubunge na udiwani. Pia, itawasaidia wananchi kuibua vipaumbele vya bajeti katika mitaa na vijiji vyao ambavyo vinasabihiana na malengo makuu ya dira ya taifa, na hivyo kushiriki kikamilifu katika kupanga maendeleo yao wenyewe.
Kwa kuzindua kampeni hii kutoka kwenye ngazi ya chini kabisa ya jamii, Sauti ya Jamii Kipunguni inajaribu kubadilisha dhana kwamba nyaraka za kisera ni za wasomi na viongozi pekee. Wanaamini kuwa maendeleo ya kweli yataletwa na wananchi watakaojua wajibu wao na kufahamu mwelekeo wa nchi yao, na hatua ya kwanza ni kuisoma na kuielewa Dira ya Maendeleo ya 2025-2050.