Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amewasilisha tathmini rasmi ya chama hicho kuhusu utendaji wa viongozi wake wakuu, akisema Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi wamefanya kazi kubwa ya kuweka misingi imara itakayoliwezesha taifa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2050. Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nungwi, Kaskazini Unguja, Balozi Migiro aliwataka wananchi kuwapa ridhaa tena ili wakamilishe kazi waliyoianza.
Akimzungumzia mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Samia, Katibu Mkuu huyo alimpongeza kwa kulinda nguzo za Muungano na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Alibainisha kuwa diplomasia ya kimkakati ya Dk. Samia, iliyojidhihirisha kupitia filamu ya "Royal Tour" na sera za kuvutia uwekezaji, imefungua milango ya fursa, na kusababisha ongezeko la watalii na uwekezaji wa kimataifa. Alisema haya yote yanajenga uchumi shindani unaohitajika kufikia Dira ya 2050.
Kwa upande wa Zanzibar, Balozi Migiro alimwelezea Dk. Hussein Mwinyi kama kiongozi wa kimapinduzi aliyefanikiwa kuleta mageuzi makubwa ndani ya muda mfupi. Alisema miradi ya miundombinu, uboreshaji wa huduma za jamii, na msisitizo wake katika uchumi wa buluu na utalii, vimeanza kuibadilisha Zanzibar na kuiweka kwenye ramani ya dunia kama kitovu cha biashara na uwekezaji.
"Sera za Dk. Mwinyi za uchumi wa buluu na utalii zimeifanya Zanzibar kuwa lulu inayong'ara kimataifa, huku zikiboresha moja kwa moja maisha ya wananchi wake," alisisitiza Balozi Migiro, ambaye ni mwanadiplomasia mbobezi.
Baada ya kuwatambulisha wagombea hao rasmi kwa wananchi, aliwahimiza wakazi wa Kaskazini Unguja na Watanzania kwa ujumla wasisite kuwapigia kura ya "ndiyo" viongozi hao. Alisema kufanya hivyo ni kuipa CCM fursa ya kubadilisha ndoto na malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo 2050 kuwa uhalisia unaoonekana na kuguswa na kila Mtanzania.