Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amewataka wanachama wa chama hicho kuwa makini na kile alichokiita njama za kutaka kukipasua chama kwa maslahi binafsi. Akizungumza na wanachama wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, mkoani Arusha, Heche alidai kuwa kuna juhudi zinazoendelea kufanywa na baadhi ya watu ili kudhoofisha chama hicho na kuzuia ajenda zake muhimu.
"Walitarajia kwamba chama hiki kingekufa, lakini tumewaonesha nchi nzima kuwa bado tuko imara. Toka tulipotoka Mlimani City, watu walifuatilia kwa umakini kwa sababu wana matumaini makubwa na CHADEMA," alisema Heche. Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi waliokuwa wakinufaika na chama kabla ya mabadiliko ya uongozi ndio wanaolete chokochoko baada ya "mirija yao ya maslahi" kukatwa.
"Baada ya viongozi wapya kuingia madarakani, wale waliokuwa wakinufaika na chama sasa wana kinyongo na wanajaribu kutuletea mgogoro. Lakini nataka kuwaambia wazi kuwa *we are not weak* (sisi si dhaifu), hatutavumilia mambo hayo," alisisitiza Heche.
Kauli hii inakuja wakati ambapo CHADEMA inaendelea kuimarisha safu yake ya uongozi na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao, huku kukiwa na mijadala mbalimbali kuhusu mustakabali wa chama hicho katika siasa za Tanzania. Heche ameonya wanachama kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaojaribu kupandikiza mbegu za mgawanyiko ndani ya chama. Amesema kuwa kuna baadhi ya watu ambao walikuwa wananufaika na nafasi zao ndani ya chama, na sasa wanajaribu kuvuruga umoja wa chama baada ya kupoteza nafasi hizo.
Heche amewataka wanachama wa CHADEMA kuwa na mshikamano na kuwapinga watu wanaojaribu kukihujumu chama. Amesema kuwa chama kiko imara na hakitakubali kuyumbishwa na watu wachache wenye maslahi binafsi. Amewataka wanachama kujikita katika kuimarisha chama na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.