Makalla Amjibu Mnyika, Asisitiza CHADEMA Yapungua Wanachama na Kupingwa na Wanachama Wenyewe Kuhusu 'Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi'

politics | Fri May 23 2025


Makalla Amjibu Mnyika, Asisitiza CHADEMA Yapungua Wanachama na Kupingwa na Wanachama Wenyewe Kuhusu 'Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi'

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amejibu madai ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwamba kaulimbiu yao ya "Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi" imepingwa na utawala. Makalla amesisitiza kuwa kaulimbiu hiyo imepingwa na wanachama wa CHADEMA wenyewe, akianza na kundi la G55, na vyama 17 vinavyotambua umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi.


Aidha, Makalla amewafahamisha CHADEMA kuwa uimara wa chama haupimwi kwa idadi ya viongozi, bali kwa idadi ya wanachama. Aliyasema hayo leo, Mei 23, 2025, mjini Shinyanga, wakati wa mkutano wa hadhara katika ziara yake ya kikazi katika mikoa saba.


Akizungumzia mkutano wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Makalla alisema: "Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, ametupa takwimu kwamba CHADEMA haina mgogoro na iko imara, lakini katika Kamati Kuu ameainisha idadi ya waliohama, akiwemo mjumbe wa Kamati Kuu na wanachama wao. Kwa hiyo, jumla ya waliohama CHADEMA ni 55. Halafu Heche anahitimisha kwa kusema CHADEMA iko imara. Nataka nimfundishe Heche kuwa uimara wa chama haupimwi kwa uongozi. Uimara au ukubwa wa chama unapimwa kwa idadi kubwa ya wanachama. Asiwadanganye watu, CHADEMA imekimbiwa na maelfu ya wanachama na inasambaratika. Hawa kifo tayari."


Makalla ameongeza kuwa amesikia kauli ya pili kutoka kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, akisema kuwa kaulimbiu yao ya "Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi" imepingwa vikali na utawala. "Ninamwambia aache uongo. Imepingwa na CHADEMA wenyewe, wakianza na G55 ambao wamepinga. Kundi la pili ni la vyama 17 vinavyotambua umuhimu wa kushiriki uchaguzi. Kundi la tatu ni la wananchi wanaotambua kuwa uchaguzi ni kwa mujibu wa katiba. Asisingizie dola," amesema Makalla.


Makalla amesisitiza kuwa CCM inaendelea kuimarika na kupata wanachama wapya kila siku, huku akidai kuwa CHADEMA inapoteza wanachama na ushawishi. Ameongeza kuwa wananchi wanaelewa umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi na hawawezi kukubali kupotoshwa na kaulimbiu za kisiasa zisizo na msingi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.