Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimeweka wazi mikakati yake ya kisiasa, huku Katibu Mkuu wake, Salum Mwalimu, akisisitiza kuwa licha ya kubezwa hapo awali, sasa wapinzani wao wanalazimika kupambana nao vikali. Akizungumza wakati wa mikutano ya Oparesheni C4C inayoendelea mkoani Katavi na Tabora, Mwalimu alieleza kuwa CHAUMMA inaendelea kujizatiti na kuwa tishio kwa wapinzani, akitabiri kuwa watachoka wakati wao wakiendelea kuimarika.
"Walitucheka, walitudharau, lakini leo hii wanapambana na sisi kwa nguvu zote. Wakati sisi tunamaliza awamu moja, wao wanaingia, jambo linaloashiria uchovu wao. Sisi tunaendelea kujaza mafuta na kujiandaa kwa awamu nyingine," alisema Mwalimu akitumia lugha ya sitiari kuonesha uimara wao.
Akifafanua kuhusu matumizi ya helikopta katika ziara zao, Mwalimu alieleza kuwa chombo hicho, kinachotumika kwa sasa katika mikoa ya Katavi na Tabora, kitarejea nchini Kenya kwa matengenezo baada ya kumaliza mizunguko ya sasa. Alisisitiza kuwa baada ya matengenezo hayo, helikopta hiyo itarejea kwa ajili ya awamu nyingine ya oparesheni, ikionyesha dhamira yao ya kuendelea na kasi ya kisiasa bila kuchoka. "Tunawaambia kuwa helikopta hii, baada ya kumaliza duru hii, itarudi Kenya kwa huduma na matengenezo, kisha itarudi tena kwa ajili ya duru nyingine kabla ya kuingia rasmi kwenye kampeni kubwa," alifafanua.
Salum Mwalimu alisisitiza kuwa mkakati mkuu wa CHAUMMA ni kutumia akili, busara, na hekima kukabiliana na changamoto za kisiasa, badala ya kutumia nguvu au maneno makali yasiyo na tija. "Tunahitaji busara kwenye nyakati ngumu, siyo ubabe. Tunahitaji akili kubwa kwenye nyakati ngumu na siyo ubabe. Tumekataa ubabe usioendana na hekima na busara. Unapokuwa na misimamo mikali, lazima uwe na mikakati na akili kubwa ya kutekeleza hiyo misimamo," alisisitiza. Kauli hii inaakisi falsafa ya chama hicho ya kujenga siasa safi na yenye tija kwa wananchi.
Aliongeza kuwa katika nyakati za majaribu na changamoto, utulivu na mipango madhubuti ndio muhimu zaidi kuliko papara au jazba. Akifafanua kwa kutumia hekima ya kidini, alisema: "Akili kubwa, hekima, busara, utulivu – vinahitajika kwenye nyakati ngumu, siyo papara, siyo maneno. Ndio maana Mwenyezi Mungu anasema kiungo cha kukiogopa kuliko vyote ni ulimi."
Oparesheni C4C ya CHAUMMA ilizinduliwa rasmi Juni 3, 2025, jijini Mwanza, na inaendelea kwa kasi katika mikoa mbalimbali, ikilenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuimarisha msingi wa chama hicho kuelekea chaguzi zijazo.