Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema wazi kuwa chama chochote cha siasa kitakachokataa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka huu kinatoa usaliti mkubwa kwa wananchi. Kauli hii nzito ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, wakati akihutubia umati mkubwa wa wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bariadi, mkoani Simiyu.
Salum Mwalimu alifafanua kuwa kitendo cha kususia uchaguzi, kwa namna yoyote ile, kinakipa nafasi chama kingine, hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupita bila upinzani mkubwa, na kwa tafsiri yake, hii ni sawa na kuwasaliti wananchi walio na matumaini na vyama vya upinzani. Alisisitiza kuwa lengo kuu la chama chochote cha siasa ni kushika hatamu za uongozi wa nchi, na ili kufanikisha hilo, ushiriki kikamilifu katika uchaguzi ni jambo la lazima.
Katibu Mkuu huyo pia alieleza umuhimu wa uchaguzi kama njia pekee ya kupata viongozi watakaowakilisha wananchi katika vyombo vya maamuzi, kama vile Bunge, ambapo sheria hutungwa, hubadilishwa au kuboreshwa kwa ajili ya masilahi na ustawi wa jamii. "Sasa unaposema hauendi kwenye uchaguzi, utawapata wapi hao viongozi wa kwenda kuwawakilisha wananchi kwenye vyombo vya maamuzi vya kuboresha mifumo na kuleta mabadiliko ya kisheria? Uliwahi kuona wapi kazi ya kuboresha mifumo ya kisheria inafanyika nje ya Bunge?" Alihoji Mwalimu akisisitiza umuhimu wa uwakilishi bungeni.
Alitumia mfano wa klabu ya mpira wa miguu akisema, "Uliona wapi klabu ya mpira iliyoanzishwa kwa ajili ya kushinda mechi na kuchukua kombe ikaacha kupeleka timu uwanjani na bado ikaendelea kuota kushinda au kuchukua kombe...!" Akimaanisha kuwa ni lazima kuingia uwanjani (uchaguzi) ili kupambana na kushinda.
Salum Mwalimu pia alionyesha kushangazwa na baadhi ya watu wanaowaita wanachama wa CHAUMMA wasaliti kwa sababu ya kuhama vyama ambavyo vinasusia uchaguzi na kujiunga na CHAUMMA. "Hivi kati yetu sisi ambao tumekubali kwenda kupambana kushiriki uchaguzi licha ya changamoto zote na wale ambao wamegoma kwenda kushiriki na wakaacha CCM ipite bila kupingwa, ni nani msaliti?" alihoji kwa ukali. Aliongeza, "Unawezaje kuacha kupambana upate wawakilishi wa kwenda kuwapigania wananchi kwa miaka yote hiyo mitano? Huko si kuwasaliti? Tangu lini fisi anasusiwa bucha?"
Akirejea historia, Mwalimu alikumbusha jinsi Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alivyowahi kuisusia CCM kwenye uchaguzi, lakini nini kilitokea? Uchaguzi uliendelea na washindi wakatangazwa. Pia alitolea mfano nchi jirani ambazo zimekuwa zikipigania mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi lakini hakuna hata siku moja waliwahi kususia uchaguzi. "Hawa watu unapowasusia wenyewe ndio anafurahi," alisema akimaanisha kuwa kususa ni kuwapa nafasi wapinzani wao. Alisisitiza kuwa CHAUMMA watapambania mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi wakiwa ndani ya mchakato wa uchaguzi. "Huwezi kusema unataka mabadiliko halafu wakati huo umekaa pembeni ya mchezo, huwezi kusema unataka ushindi wakati uko nje...unatakiwa kuingia ndani ya mchezo ndio upambanie ushindi wako," alihitimisha Salum Mwalimu.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mwenyekiti Bara wa CHAUMMA, Bi. Devotha Minja, alithibitisha kuwa chama chao kimejipanga kikamilifu kusimamisha mgombea urais mwenye nguvu kubwa ya kisiasa, ambaye ana uwezo wa kutosha kupambana na mgombea wa CCM. Aidha, Bi. Minja alisisitiza kuwa chama kimejipanga kusimamisha wagombea nchi nzima katika nafasi za Ubunge na Udiwani. Alimalizia kwa kutangaza kuwa wiki ijayo, chama kitatangaza ratiba kamili ya kuchukua na kurejesha fomu kwa wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani. CHAUMMA inaendelea na ziara zake mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa operesheni yake maalum ya C4C.