Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Mhe. Hassan Bomboko, amefungua ukurasa mpya wa utendaji katika wilaya hiyo kwa kutoa maagizo mazito yanayolenga kuondoa "uoga" wa kimaendeleo. Katika kile kinachoonekana kama kuamsha ari ya kujitegemea, Bomboko ameielekeza Halmashauri ya Wilaya hiyo kuacha kufikiria miradi midogo midogo na badala yake wajipange kubuni na kutekeleza miradi ya ujenzi yenye thamani inayoanzia Shilingi Bilioni Moja kwa kutumia mapato yao wenyewe ya ndani.
Agizo hilo "nzito" limetolewa leo, Novemba 25, 2025, katika viunga vya ofisi za halmashauri hiyo wakati wa hafla ya kihistoria ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Jengo la Utawala la kisasa (Headquarters). Mradi huo mkubwa unatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 4.39 na utatekelezwa na kampuni ya uzalendo ya PARIK Limited yenye makao yake mjini Moshi.
"Hakuna Nafasi kwa Wakandarasi 'Kanjanja'" Akizungumza kwa lugha ya picha na msisitizo, DC Bomboko aligeukia Kitengo cha Manunuzi (PMU) na kuwataka kuwa "mbogo" dhidi ya wakandarasi wababaishaji. Alionya kuwa zama za kupeana kazi kwa kujuana au "giza giza" zimepitwa na wakati na serikali haitavumilia kuona miradi inakwama kwa sababu ya kuwapa kazi watu wasio na uwezo wa kifedha wala kiufundi.
"Tunakoelekea sasa ni kubaya kwa wazembe. Hatutaki kufika kwenye 'site' tukakuta hata miradi ya 'Force Account' inasuasua kwa sababu msimamizi hana uwezo. PMU chakatauni na leteni wakandarasi sahihi. Tufanye kazi kwa uwazi, tushirikishane. Mambo ya kufanya kazi gizani hayana nafasi katika awamu hii," alisisitiza Bomboko.
Uzalendo na Uwajibikaji: "Jengeni Kama Nyumba Zenu" Mkuu huyo wa Wilaya alienda mbali zaidi kwa kugusia suala la 'ownership' (umiliki) wa miradi ya umma. Aliwataka watendaji na wasimamizi wa mradi huo kutofanya kazi kwa hofu ya kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) au kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru ndipo wapakare rangi majengo, bali wafanye kazi kwa weledi wakitambua kuwa hiyo ni mali yao na ya vizazi vijavyo.
"Tufanye miradi hii kana kwamba tunajenga nyumba zetu wenyewe za kuishi na familia zetu. Huu ndio uzalendo tunaoutaka. Tusisubiri kusukumwa na wakaguzi, tujisimamie wenyewe," aliongeza.
Ofisi Mpya: Mwarobaini wa Msongamano Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Dionis Myinga, alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo jipya ni hitaji la lazima na si anasa. Alibainisha kuwa jengo la sasa limezidiwa na idadi ya watumishi na kuongezeka kwa idara na divisheni mbalimbali, jambo linaloathiri ufanisi wa kazi.
"Tunamshukuru Mungu na Serikali Kuu, Wizara imetuidhinishia Shilingi Bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi huu. Sisi kama Halmashauri tumefuata taratibu zote za kisheria za manunuzi na leo tunasaini mkataba rasmi ili kazi ianze mara moja," alisema Myinga.
Kwa upande wa kiufundi, Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo, Anold Matandiko, alibainisha kuwa mradi huo ni wa miezi 24 (miaka miwili). Alithibitisha kuwa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la kazi (site possession) kuanzia leo Novemba 25, 2025 na anatarajiwa kukabidhi funguo za jengo hilo lililokamilika ifikapo Novemba 25, 2027.
Ujenzi wa jengo hili unatazamwa kama hatua kubwa kwa Wilaya ya Hai katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi, huku maagizo ya DC Bomboko yakitarajiwa kuamsha ari ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha miradi mikubwa zaidi siku za usoni.