Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha kuwa mchakato wa ugawaji wa majimbo ya uchaguzi unazingatia vigezo muhimu kama vile idadi ya watu, jiografia, upatikanaji wa huduma za kijamii, na maendeleo ya kiuchumi. Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu kutoka chama hicho, Petro Ndolezi, amesisitiza kuwa ugawaji huo usifanywe kwa maslahi binafsi au ya kisiasa.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Ndolezi alieleza kuwa mchakato huo unapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi. Alikumbusha kuwa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaitambua Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambayo hapo awali ilijulikana kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Sheria Namba 2 ya mwaka 2024.
Ndolezi alionyesha wasiwasi wake kuhusu ukosefu wa uwiano katika uwakilishi wa majimbo. Alifafanua kuwa Tanzania Bara ina majimbo 214, lakini mgawanyo wake haujazingatia usawa wa idadi ya watu. Alitoa mifano mbalimbali kuonyesha tofauti kubwa katika ukubwa wa majimbo na idadi ya watu wanaowakilisha.
Alilinganisha Mkoa wa Kigoma, wenye majimbo 8 na idadi ya watu 2,470,967 katika eneo la 45,066 km², na Mkoa wa Mtwara, wenye majimbo 10 lakini idadi ndogo ya watu 1,634,947 katika eneo dogo la 16,710 km². Alitolea mfano Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, ambayo ina eneo kubwa la 28,901 km² (kubwa kuliko Mkoa mzima wa Mtwara), lakini ina jimbo moja tu la uchaguzi (Kigoma Kusini).
Ndolezi pia aligusia Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ambayo ina majimbo matatu (Lulindi, Masasi, na Ndanda) kwa wakazi 314,778, wakati Jimbo la Kigoma Kusini pekee lina wakazi 458,353 lakini halijagawanywa. Aliongeza kuwa majimbo ya Kigoma Kusini na Kasulu Vijijini yana jumla ya wakazi 537,767 lakini hayajagawanywa, huku majimbo mengine yenye idadi ndogo ya watu yakiwa na uwakilishi mkubwa zaidi.
Akitoa mfano mwingine wa uwiano usio sawa, Ndolezi alitaja Jimbo la Pangani mkoani Tanga, lenye wakazi 75,645 na mwakilishi mmoja bungeni, huku Kata ya Murungu katika Jimbo la Muhambwe (Kigoma) ikiwa na wakazi 84,449 lakini ikiwakilishwa na diwani mmoja tu. "Hii ina maana mbunge wa Pangani anawakilisha watu wachache kuliko diwani wa Kata ya Murungu. Hakuna usawa katika uwakilishi," alisisitiza Ndolezi.
ACT Wazalendo imesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika ugawaji wa majimbo ili kuhakikisha uwiano wa idadi ya watu, jiografia, na mahitaji ya maendeleo ya wananchi unazingatiwa. Ndolezi ameihimiza serikali na INEC kufanya tafiti za kina kabla ya kugawa majimbo mapya ili kuhakikisha uwakilishi bungeni unakuwa wa haki na uwiano.